27.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Siku 52 za kampeni vifo 11

NA AZIZA MASOUD, DAR ES SALAAM

TANGU kampeni za Uchaguzi Mkuu zianze Agosti 22 mwaka huu, hadi kufikia jana jumla ya wagombea 11 wamefariki dunia.

Vifo hivyo vimewakumba wagombea mbalimbali wa nafasi za ubunge na udiwani kutoka vyama vya CCM, muungano wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) pamoja na Chama cha ACT- Wazalendo.

Mfululizo wa matukio ya vifo vya wagombea wa nafasi hizo katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, ni dhahiri umeitikisa jamii kwa kiasi kikubwa.

Dadisi mbalimbali zinatanabaisha kwamba, mfululizo wa matukio ya vifo vya wagombea wa ngazi za ubunge na udiwani haujawahi kutokea katika historia ya nchi tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1995.

Kwamba ndani ya kipindi cha takribani mwezi mmoja na nusu sasa matukio yote hayo yametokea kwa sababu mbalimbali ikiwamo maradhi na ajali.

Kwa mfano Septemba 12 mwaka huu, mgombea ubunge wa Jimbo la Korogwe  kupitia Chadema chini ya mwavuli wa Ukawa, Mohammed Mtoi, alifariki dunia kwa ajali mbaya ya gari katika eneo la Magamba wilayani Lushoto.

Mauti yalimkuta Mtoi wakati akirudi kutoka katika kampeni zake ndani ya Jimbo la Lushoto ambalo alikuwa akiliwania.

Septemba 24, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Celina Kombani, naye alifariki dunia wakati akiwa kwenye matibabu huko nchini India.

Marehemu Kombani alikuwa anatetea nafasi yake ya ubunge katika Jimbo la Ulanga Mashariki kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Siku chache baada ya kifo cha Kombani, Oktoba 9, mgombea ubunge wa Jimbo la Arusha Mjini kupitia Chama cha ACT- Wazalendo, Estomih Malla, alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC iliyopo mkoani Kilimanjaro.

Tukio hilo lilifuatiwa na kifo cha mgombea ubunge aliyekuwa anatetea kiti chake katika Jimbo la Handeni Mjini kwa tiketi ya CCM, Dk. Abdallah Kigoda ambaye alifariki dunia Oktoba 12 wakati akipatiwa matibabu nchini India.

Kabla ya mauti kumkuta, marehemu Dk. Kigoda, alikuwa ni Waziri wa Viwanda na Biashara.

Siku chache baada ya msiba huo, juzi Mwenyekiti mwenza wa Ukawa, Dk. Emmanuel Makaidi, alifariki dunia wakati wakipatiwa matibabu katika Hospitali ya Ngao mkoani Lindi.

Dk. Makaidi wakati anakutwa na mauti hayo alikuwa ni Mwenyekiti wa Chama cha National League for Democracy (NLD), pia alikuwa mgombea ubunge wa Jimbo la Masasi.

Kifo cha Dk. Makaidi kilifuatiwa saa chache na kifo cha mgombea ubunge ambaye alikuwa anatetea kiti chake katika Jimbo la Ludewa, Deo Filikunjombe.

Marehemu Filikunjombe alikutwa na mauti wakati akiwa safarini kurejea jimboni mwake akitumia usafiri wa helikopta ambayo ilipata ajali na kuanguka katika mbuga ya wanyama ya Selous mkoani Morogoro.

Mbali na vifo vya wagombea wa ubunge, pia ndani ya kipindi hicho cha kampeni jumla ya madiwani watano wa kata mbalimbali nao walifariki dunia kwa sababu mbalimbali.

Miongoni mwao ni mgombea udiwani wa Kata ya Muleba wilayani Muleba, Osward Rwabaka na mgombea udiwani wa Kata ya Uyole jijini Mbeya ambao wote walikuwa wanawania nafasi hiyo kupitia CCM.

Mbali na vifo hivyo vya wagombea, kifo cha mwanasiasa Mchungaji Christopher Mtikila kilichotokea Oktoba 4 mwaka huu, nacho kimeweka kumbukumbu ya aina yake katika uchaguzi wa mwaka huu.

Ikumbukwe mwaka 2005 mgombea mwenza wa Chadema, Jumbe Rajab Jumbe, alifariki dunia katika kipindi cha kampeni hivyo Tume ya Taifa ya Uchaguzi kusogeza mbele uchaguzi mkuu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles