23.7 C
Dar es Salaam
Sunday, October 1, 2023

Contact us: [email protected]

Mkapa: CCM ikishindwa dunia itashitushwa

g1Amina Omari na Oscar Assenga, TANGA

RAIS mstaafu, Benjamin Mkapa amesema iwapo Chama Cha Mapinduzi (CCM) kitashindwa kushika dola katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika siku nane kuanzia leo, dunia nzima itashitushwa kutoka na chama hicho kuwa na misingi imara ya uongozi.

Kauli hiyo aliitoa mjini hapa jana, katika Viwanja vya Tangamano wakati wa mkutano wa hadhara wa kumnadi mgombea ubunge wa Jimbo la Tanga Mjini kupitia chama hicho, Omari Nundu na madiwani wa kata 27.

Alisema itakuwa ni maajabu na ulimwengu utashangazwa nchi hii kuongozwa na viongozi ambao vyama vyao ni vichanga na hawana sera.

Alisema vyama vya upinzani bado ni vichanga kuweza kutawala kwa kuwa bado hawana uwezo wa uongozi kutokana na kutokuwa na sera wa dira ya kuleta mabadiliko ya ukweli ndani ya nchi hii.

“Kwa jinsi Serikali ya CCM inavyoheshimika dunia leo hii mataifa makubwa na nchi nyingi za Afrika wanategemea mawazo na busara za viongozi wa chama hicho ambao ni waadilifu na mahiri katika kusaidia nchi mbalimbali,” alisema.

Mkapa alisema nchi hii inahitaji kuongozwa na mtu ambaye ni muadilifu na mchapakazi atakayeweza kutuletea maendeleo makubwa na mtu huyo ni mgombea urais wa chama hicho, Dk. John Magufuli.

Pia aliwabeza baadhi ya wagombea wa vyama vya upinzani kuwa wengi wao wanatafuta heshima ya kuongozwa na pikipiki na kupigiwa mizinga.

Alihoji iwapo wapinzani watapewa nchi watakwenda kutekeleza sera za nani, kwa kuwa hawana ilani wala sera zinazoweza kutoa dira ya kuwaletea mafanikio wananchi.

“Ninasema Magufuli ni mwadilifu kwa sababu katika bajeti ya Serikali, Wizara ya Ujenzi aliyokuwa akiiongoza inatengewa bajeti kubwa na ameweza kuisimamia vizuri, huyo ndiye kiongozi tumtakaye katika nchi hii,” alisema Mkapa.

“Ninawashangaa wenzangu, licha ya mazuri ambayo Serikali katika awamu zake mbalimbali imefanya, bado wanasema hakuna kitu, hivi hao mnaweza kuwachagua ikiwa waliweza kushiriki kuleta mabadiliko kisha wanayakana wenyewe,” alisema Mkapa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga, Henry Shekifu, alimfananisha Magufuli na Nuhu aliyeteuliwa ili kuwakomboa Watanzania.

“Mungu alipoona watu wake wanapata shida aliweza kumtuma mtume Nuhu ili aweze kuleta ukombozi, hivyo Watanzania kwa ujumla Magufuli ndiyo mfano huo,” alisema Shekifu.

Naye Nundu alisema ana imani wananchi wa jimbo hilo hawataweza kumuangusha katika kipindi hiki kingine.

Alisema ameweza kufanya makubwa katika kutekeleza na kuisimamia ilani ya CCM kwa mafanikio makubwa, licha ya wapinzani kuendelea kuyabeza maendeleo hayo.

  1. MAGUFULI AUNGURUMA ZANZIBAR

 

Kutoka Zanzibar, mwandishi wetu anaripoti kuwa Dk. Magufuli amemaliza ziara ya kampeni hapa zake kisiwani humo na kuweka historia ya kuwa mgombea aliyepata idadi kubwa ya watu katika mikutano yake.

Mkutano wake ulifanyika jana katika Viwanja vya Mnazi Mmoja na kuhudhuriwa na maelfu ya Wazanzibari.

 

Akihutubia katika mkutano huo, Dk. Magufuli aliwahakikishia Wazanzibari kuwa akichaguliwa atakuwa rais wa Watanzania wote na amepata imani kubwa kuwa watamchagua kutokana na mapokezi makubwa aliyopata.

“Nimesimama hapa kuomba kura, nina imani na nyinyi kwa kuwa mimi nimedhamiria kuwatumikia wananchi wa Tanzania bila ubaguzi,” alisema Dk. Magufuli.

Aliahidi kupambana na rushwa na vitendo vya uharamia na uvuvi haramu katika bahari kuu kwa kuimarisha ulinzi.

“Hapa ni kazi tu, nitawashughulikia mafisadi wote nikiingia madarakani na ndiyo maana nilipopitishwa tu na chama kugombea nafasi hii mafisadi wote waliondoka CCM,” alisema Dk. Magufuli.

Pia alisisitiza umuhimu wa kuendeleza amani ya nchi ili Tanzania iendelee kuwa tulivu na kukaribisha wageni zaidi, wakiwemo watalii wanaoleta fedha za kigeni.

“Pasipo amani hakuna anayeweza kufungua duka, hakuna mtalii atakayekuja kutembelea Bara wala Zanzibar, hakuna mtu atakayekuja kujifunza historia ya Zanzibar ambayo inatajika ulimwenguni kote,” alisema Dk. Magufuli.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles