30.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, December 17, 2024

Contact us: [email protected]

Siku 39 za tetemeko, Rais Magufuli hujakanyaga  Kagera!

rais-akipiga-pushapuWAHAYA wana methali isemayo: ‘‘Atashuliza ajunza” Tafsiri ya methali hii kwa Kiswahili ni kwamba mtu asiye na tabia ya kukagua vitu vyake huruhusu vioze au viharibike.

Methali hii hutufundisha kuwa ni muhimu kuwa na tabia ya kukagua ulipoweka mali yako, au kufuatilia mambo yako ya muhimu au vitu vyako vya thamani. Vinginevyo utakuta vimekwisha haribika au vimeporwa.

Ikiwa imetimia takribani siku 39 sawa na masaa 936 yenye  dakika 56,160 ambazo ni sekunde 336,9600 wakazi wa mkoa wa Kagera bado wana majonzi wasijue la kufanya kutokana na janga la tetemeko la ardhi.

Tetemeko ambalo lilishtua Taifa, Bara la Afrika na dunia kwa ujumla ukizingatia nchi yetu haikuwahi kushuhudia  matetemeko makubwa kufikia hadi kipimo cha Richter 5.7 ambayo kimsingi huwa tunayasikia kwenye mabara mengine hususani Asia.

Ajabu na kusikitisha tangu tukio hili la kuogopesha litokee, Rais wetu, Dk.. John Pombe Magufuli hakuwahi  kukanyaga katika ardhi ya Kagera, zaidi ya  kumtuma Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Ni kweli baada ya tukio Rais alionyesha uzalendo kwa kuahirisha safari yake  kwenda  Zambia kushuhudia kuapishwa kwa Rais, Edgar Lungu,  lakini hiyo haitoshi ukizingatia kutokwenda mara kwa mara nje ya nchi siyo vipaumbele vyake  kama njia mojawapo ya  kubana matumizi yasiyo ya lazima.

Ni dhahiri pamoja na majukumu makubwa uliyonayo Rais,  lakini  ukiwa kiongozi mkuu wa nchi ulitakiwa kufika mkoani Kagera mapema iwezekanavyo ili kuwapa pole waliojeruhiwa na kuwafariji waliofiwa kutokana na tetemeko hilo kabla ya kiongozi mwingine kwenda.

Ikumbukwe kuwa wapo mahasimu wako kisiasa hasa kutoka vyama vya upinzani walifika mapema katika tukio huku wakianza kutoa kasoro za kiutendaji wa Serikali yako kwa kushindwa kushughulikia haraka mkasa huu.

Ni ukweli usiopingika Rais ukiwa na wewe ni binadamu mwenye mwili wa damu na nyama tena uliojaa nyongo, hali ya kukosolewa namna hiyo ilikukera hadi ukaanza kulalamika kwa kusema wanasiasa wasitumie janga hili kama mtaji wao  kisiasa maana si Serikali wala  CCM iliyosababisha maafa haya.

Kiukweli ilitakiwa iwe hivyo maana katika siasa vyama vya upinzani hujitafutia fursa na kujiimarisha kwa kutumia udhaifu wa Serikali. Hata hivyo ulitaka wapinzani wako  wafanye nini kama wewe Rais  ulishindwa kuwahi katika eneo la tukio kabla sumu haijamwagwa?

Sawa, umejitahidi kukusanya michango kwa ajili ya wahanga na hivyo unastahili pongezi, lakini  haitoshi maana Kagera  kuna shinda nyingi ambapo wapo  wanaolalamika kuwa hawajawahi kupewa misaada huku wengine wakisema inatolewa kwa upendeleo.

Mheshimwa Rais, ni vioja kama unahamasika kutoa msaada wa kipekee kwa mama mjane baada ya kusikia shida zake kupitia luninga. Kumbuka huyo ni mmoja ila wapo wajane na masikini wengi ambao  hawajatolewa taarifa kupitia vyombo vya habari.

Ili kuwajenga kisaikolojia wakazi wa Kagera wasiendelee  kujihisi umewanyanyapaa hutaki kwenda kule wakulilie shida zao kama wewe ulivyowalilia wakupe kura mpaka ukapiga pushapu, Mheshimiwa Rais  chukua hatua kabla wapiga kura wako hawajaharibika au kuporwa.

Pamoja na kuwa Serikali haiwezi kufanya kila kitu, lakini si busara kutoa kauli za kuwaumiza akili kwa kuwaambia Wanakagera  kuwa Serikali haikusababisha maafa hivyo  wajitafutie ufumbuzi wakati ukijua wao hutegemea zaidi  mazao ya mibuni na migomba ambayo siku hizi yako taabani huku ukame mkubwa ukiwakumba.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles