27.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Sikiliza mtazamo wa mtoto hata kama haukubaliani nao

Na CHRISTIAN BWAYA

UZOEFU unaonesha kuwa familia zinazokuwa na tamaduni zinazofahamika bayana kwa kila mwanafamilia, zina uwezekano mkubwa zaidi wa kuwa na upendo, nidhamu na uwajibikaji. Haya matatu ndiyo yanayojenga hali ya upendo katika familia, mshikamano na ukaribu zaidi kuliko familia zisizo na misingi iliyo bayana. Tunapozungumzia utamaduni wa familia, tunamaanisha tabia na mienendo inayotarajiwa kwa kila mwanafamilia. Kwa kawaida, tabia hizi hugeuka kuwa sawa na sheria na kanuni zinazoongoza taasisi tunazofanyia kazi. 

Utamaduni wa familia unapofahamika kwa kila mwanafamilia huambatana na faida kubwa mbili. Kwanza, ni kumsaidia kila mwanafamilia kuelewa yeye ni nani, nafasi yake katika familia ni ipi, anatakiwa kufanya nini na kipi hapaswi kukifanya kama sehemu ya familia. Lakini pia, kila mwanafamilia anapojitambua na kuelewa nafasi yake katika familia, inakuwa rahisi kwa wazazi kujenga mtazamo wa pamoja unaoongoza malengo ya familia. 

Kama tulivyogusia kwenye makala iliyopita, mamlaka ya juu katika familia ni wazazi. Maisha ya mzazi mwenyewe ndiyo yanayojenga matarajio yanayoongoza mienendo ya watoto. Kile unachokifanya mzazi ndicho kinachoigwa na mtoto. Unapokuwa na tabia ya kuwasalimia watoto kila asubuhi, kwa mfano, kwao huo ndio unakuwa utamaduni wao. Hawataacha kusalimia kwa sababu wanajua hawataeleweka. Kwa hiyo ni muhimu kuwa makini na vile unavyoishi. Chochote unachokifanya ndicho kinachogeuzwa kuwa sheria na wanao na ndicho kitakachokuwa utamaduni wa familia yako. Hii ndiyo sababu wakati mwingine mtoto anakuwa na tabia fulani zisizofaa lakini hakuna mtu anaweza kuwaonya wakabadilika kwa sababu wameona wazazi wao wakifanya hicho wanachokifanya. 

Kwa kuwa wazazi nao ni kama wanadamu wengine, hukosea wakati mwingine bila wao wenyewe kujua, ni muhimu kufanya mazungumzo shirikishi ili kukusaidia kuona vile watoto wanavyokuona. Kwa muktadha huu, mazungumzo ya pamoja yanakusaidia kuweka misingi itakayotumika kusaili mwenendo wa yeyote akiwemo mzazi mwenyewe. Faida ya kufanya hivi ni kumsaidia hata mzazi mwenyewe kujikosoa na kujirekebisha pale anapokwenda kinyume na misingi inayokubalika kwenye familia.

Kama nilivyogusia kwenye makala iliyopita, wakati mwingine wazazi hufikiri watoto hawana uelewa wa kujua wanahitaji nini na hivyo kudhani kuwa kazi yao ni kufuata kile walichokiamua wao. Matokeo yake ni kwamba watoto huwa kinyume na kile wanachoamini wanatakiwa kukifanya. Lakini ukweli ni kwamba ukiweza kuwa karibu na mtoto na ukamfanya ajisikie kueleweka, anaweza kukueleza vizuri kile anachokiona na ukapata mahali pa kuanzia unapojenga utaratibu wa kufuatwa katika familia. 

Unapozungumza na mtoto anza kwa kupata mrejesho wake kadri inavyowezekana. Jitahidi kusikiliza mtazamo wake hata kama hukubaliani nao. Kwa kawaida ni rahisi kumbadilisha mtu anayeamini unamsikiliza kuliko kumdhibiti mtu asiyeamini unamsikiliza. Kwahiyo, fanya juhudi za kumsikiliza mtoto bila kujali kiwango cha uelewa wake. Muulize maoni yake kuhusu uhusiano wake na wazazi, tabia anazotamani kuziona nyumbani na mambo kama hayo. Kisha muulize vitu gani havimpendezi anapoona vinafanyika. Najua kwa mzazi mijadala kama hii inaweza kuwa na ugumu wake. Lakini unapokuwa na kifua cha kupata mtazamo wake itakusaidia kujua anafikiri nini, anatamani nini, anahofia nini na hiyo itakusaidia kujua wapi pa kuanzia unapojenga utamaduni wa familia ambao kila mwanafamilia anajiona kuwa sehemu yake.

Christian Bwaya ni Mhadhiri wa Saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU). Mawasiliano 0754870815, twitter: @bwaya

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles