32.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Sifa zipi mwanamume huzitafuta kwa mwenzi wake? -2

9-tips-to-save-your-rocky-relationship-9

Na CHRISTIAN BWAYA,

TULIONA katika makala iliyopita kuwa mwanamume anahitaji kutambuliwa uwezo wake. Huna sababu ya kumwambia mwanamume unampenda. Lugha ya upendo anayoielewa zaidi ni kusifiwa uwezo wake. Sambamba na hili la kwanza, tuliona mwanamume anayo njaa ya heshima. Heshima ni kumtii na kumstahi hata pale anapokuwa mkosaji kwa lugha, maneno na tabia.

Makala ya leo inaangazia mahitaji mengine mawili yanayogusa moyo wa mwanamume.

Anatamani kusikilizwa, si kukosolewa
Wanaume wengi hawapendi kukosolewa hata kama hawasemi. Unapomkosoa mwanamume unamfanya apoteze hali ya kujiamini na hivyo hujisikia kama mtu anayeongozwa. Si wanaume wengi hufurahia kuongozwa. Kinyume na kumkosoa, ifanye sauti yake isikike.
Tuchukulie mfano kuwa mwenzi wako amekuja na wazo la kufanya jambo fulani analodhani ni muhimu mlitekeleze. Kwa mwanamke msomi mwenye uwezo wa kuchambua mambo, wakati mwingine ni rahisi kubaini kwa haraka hitilafu ya pendekezo analolitoa.

Kwa haraka, unaweza kuonesha upinzani wa wazi wazi kuwa kinachopendekezwa hakina mashiko. Si wanaume wengi wanaweza kuvumilia kuonekana wana mawazo yasiyo na mashiko hata kama ni kweli.

Hulka ya mwanamume kutamani kuwa na sauti, inaweza kumfanya aamue kusisitiza wazo lake akiamini ana haki ya kuungwa mkono. Si busara hata kidogo kumpinga wazi wazi kwa lugha inayolenga kuonesha upungufu wake. Kufanya hivyo kunamnyong’onyeza, hali ambayo hatakubali itokee.
Ikiwa unataka kukamata moyo wa mwanamume, jifunze kushuka na kumtanguliza katika uamuzi. Linda hadhi ya mume wako kwa kuonesha heshima kwa mawazo yake. Ukiweza kugusa moyo wake kwa kuonesha umuhimu wa anachokisema, itakuwa rahisi kutoa pendekezo lako kwa namna ambayo ni rahisi kupokelewa.

Anahitaji uhuru, faragha
Uhuru na faragha kwa hakika ni kinyume kabisa na kile ambacho wanawake wanakihitaji kama tutakavyoona mbeleni. Lakini kwa mwanamume, ukweli ni kuwa anahitaji kujiona ni mtu mwenye uhuru wa kufanya mambo anayoyafurahia bila kuambiwa kingine cha tofauti anapaswa kukifanya.

Kwa mfano; kama mume wako anapenda mpira, ukweli ni kuwa anatamani umpe ushirikino. Ukiweza kujitahidi kufurahia mpira utagusa moyo wake kwa namna ya tofauti. Chochote anachopenda kukifanya mume wako wakati wa muda wake wa ziada, mpe nafasi ya kuwa yeye bila kumwingilia isipokuwa inapokuwa ni lazima.

Kama anayo mambo anayoyapenda na hayaharibu maisha yenu, jiunge nae. Isipowezekana, mpe uhuru wa kupenda mambo yake. Huna sababu ya kumfanya aachane na marafiki zake kama hawaathiri uhusiano wenu. Huna sababu ya kumfanya aache kwenda maeneo anayoyapenda ikiwa kufanya hivyo hakuleti madhara. Mpe nafasi ya kuwa huru.

Kadhalika, uhuru unakwenda sambamba na kuhitaji faragha. Kimsingi, kama mwanamke saa nyingine unatamani ufahamu kila anachokifanya mume wako. Unahitaji kujua mawasiliano yake, ameongea na nani, ameandikiana na nani, anafahamiana na nani na ikiwezekana ujue kila nukta ya mawazo yake. Pengine unaweza hata kushawishika kumchunguza kwa siri.

Hata hivyo, kwa wanaume wengi jambo hili halipendezi. Wanaume wanatamani kuwa na nafasi ya kufanya mambo yao bila kupelelezwa. Hawapendi kuona wakinyang’anywa haki ya kuwa na faragha.

Ikiwa unatamani kuwa na uhusiano uliojengwa katika msingi wa kuaminiana, mfanye akuamini ili kwa utashi wake akuruhusu kuingilia maisha yake ya faragha kwa hiari yake. Kadri anavyokuamini ndivyo anavyoweza kukukabidhi uhuru unaoutaka wewe bila kuleta mtafaruku.
Itaendelea…

Mwandishi ni Mhadhiri wa Saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge. Blogu: http://bwaya.blogspot.com , 0754 870 815

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles