26.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 17, 2024

Contact us: [email protected]

Kilichoushinda ulimwengu Rwanda kinajirudia Syria?

Mapigano Syria yanahusisha pande zenye malengo tofauti zikisaidiwa na mataifa makubwa yenye masilahi tofauti
Mapigano Syria yanahusisha pande zenye malengo tofauti zikisaidiwa na mataifa makubwa yenye masilahi tofauti

MAUAJI ya kutisha nchini Rwanda mwanzoni mwa miaka ya 1990, ni moja ya majinamizi mabaya zaidi yanayoendelea kuusumbua Umoja wa Mataifa (UN) na Magharibi hadi leo hii na haijulikani bado lini taswira hii mbaya itafutika.

Aliyekuwa Rais wa Marekani wakati huo, Bill Clinton, aliwahi kuiita kesi hii kama tukio moja kubwa kabisa analolijutia wakati wa urais wake.

Ndiyo maana si ajabu baada ya kustaafu kwake, shughuli zake nyingi za kibinadamu za taasisi yake ya Clinton Foundation zimejikita nchini humo.

Vita ya wenyewe kwa wenyewe ya Rwanda mwaka 1990 ilishuhudia kundi la waasi wanaoongozwa na Watutsi chini ya Paul Kagame, Rwandan Patriotic Front (RPF) kutokea ukimbizini Uganda, wakipambana na Serikali ya Rwanda ya Rais Juvenal Habyarimana, ambaye ni Mhutu.

Malengo ya RPF yalikuwa kuiangusha serikali iliyokuwa ikiungwa mkono na Ufaransa pamoja na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) wakati huo ikijulikana  kama Zaire. RPF ilikuwa ikidhibiti eneo dogo tu la kaskazini mwa nchi.

Baada ya miaka kadhaa ya majadiliano, makubaliano ya amani yakafikiwa mjini Arusha, Tanzania Agosti 1993, ambayo kama kawaida yaliipa UN jukumu la kulinda amani kwa kupeleka jeshi la kimataifa lisiloegemea upande wowote.

Jukumu la jeshi hilo lilikuwa pamoja na kusaidia utekelezaji wa makubaliano hayo, kulinda mji mkuu wa Kigali na kutengeneza jeshi linalojumuisha pande zote mbili hasimu pamoja na kubwa; kuhakikisha usalama wa raia.

Hata hivyo, wiki tu baada ya kusainiwa, kulikuwa na ripoti nyingi zikiwamo kutoka Tume ya UN ya  Haki za Binadamu, ikionesha uwapo wa machinjo ya kutisha na ukiukaji mwingine wa haki za binadamu nchini humo zaidi ukiwalenga Watutsi na Wahutu wenye msimamo wa wastani.

Licha ya yote hayo, UN na jumuiya ya kimataifa zikiongozwa na Magharibi zilionekana kupuuza au kuwa nzito kuchukua hatua kana kwamba Wanyarwanda si watu wanaostahili ubinadamu.

Mbaya zaidi UN mara kadhaa ilikuwa ikitishia kuondoa askari wake wachache iwapo Habyarimana hatadhibiti mauaji na uhalifu mwingine ilihali ikifahamu fika rais huyo hakuwa na nguvu za kuwadhibiti Wahutu wenzake.

Hali ikawa mbaya zaidi kuanzia Aprili 6, 1994 wakati ndege iliyombeba Rais Habyarimana na mwenzake wa Burundi ilipotunguliwa wakati ikitokea Tanzania. Upande uliohusika na uhalifu huo ni kitendawili na umekuwa ukizikosanisha Ufaransa na Serikali ya Kagame hadi leo hii.

Hivyo, yakaanza machinjo ya kutisha ya kimbari ya siku 100, ambayo watu zaidi ya 800,000 waliuawa mbele ya macho ya UN, ambao walikuwa wakitizama tu.

Miongoni mwa matukio ya kusikitishwa ni pale aliyekuwa Waziri Mkuu Agathe Uwilingiyimana, maarufu kwa jina la Madame Agathe alipouawa kesho yake.

Madame Agathe, Waziri Mkuu wa kwanza mwanamke nchini humo alikuwa amekimbilia kujificha katika kambi iliyokuwa ikilindwa na UN kwa ajili ya kuhifadhi wakimbizi wa ndani.

Lakini hilo halikuzuia wanamgambo wenye msimamo mkali kumsaka na walimkuta amejificha, wakamwua kikatili papo hapo, mauaji yaliyoendelea kwa siku nyingine 98 kabla ya akina Kagame kuikamata nchi hiyo.

Unyama huo, kwa sasa unatokea nchini Syria, huku mataifa makubwa yakibakia kuvutana wao kwa wao juu ya namna ya kuumaliza mgogoro huo, kila upande unaonekana kuwekeza kwanza maslahi yake kabla ya raia.

Hali mbaya zaidi iko katika mji wa Aleppo, ambako raia wanaendelea kushuhudia mashambulizi ya angani, ardhini na makombora.

Raia hawa kwa masikitiko makubwa wanajiuliza wameukosea nini ulimwengu na umechukua jukumu gani katika kuwalinda dhidi ya vitisho.

Mikataba ya Geneva na ya Baraza la Usalama la UN ilianzishwa baada ya Vita Kuu ya Pili ili kudumisha amani na kuwalinda watu walioko maeneo ya vita. Lakini mikataba hiyo inaonekana kuwa na ufanisi mdogo.

Miongoni mwa mikataba hiyo ya Geneva ni pamoja na kanuni ya R2P iliyoanzishwa na mataifa wanachama UN, ili kuzuia mauji ya halaiki.

Kanuni hiyo ilianza kutumika rasmi mwaka 2005 kufuatia funzo lililotokana na mauji ya kimbari ya Rwanda 1994.

Kanuni hiyo pia ililenga kuzuia kutokea tena mauaji kama ya mwaka 1995, yaliyoendeshwa na vikosi vya Serbia katika mji wa Srebrenica dhidi ya wanaume na wavulana wa Kibosnia 8,000 wa dini ya Kiislamu.

Lakini kanuni hiyo ya UN ya kuwalinda raia inaonekana kutofanikiwa, kwa mujibu wa Mbunge wa Uingereza, Paddy Ashdown ambae aliwahi kuwa mwakilishi wa Bosnia na Herzegovina kati ya mwaka 2002-2006.

Ashdown ambaye alikuwa miongoni mwa wanasiasa wa Magharibi waliotoa wito wa kuingilia kijeshi vita vya Bosnia katika miaka ya 1990, anasema ulimwengu umekuwa ukisita kujihusisha katika machafuko yanayotokana na migogoro ya muda mrefu.

Vita ambavyo vimetokea tangu vile vilivyoongozwa na Marekani nchini Irak mwaka 2003, vimeonyesha kuwa mataifa ya Magharibi hayawezi kuibuka na mikakati mwafaka ya kuwalinda raia, aliongeza mwanasisa huyo wa Uingereza.

Nchini Libya, miaka minane baadae Marekani, Uingereza na washirika wao zimekosolewa kushindwa kuleta amani baada ya kuondolewa madarakani kwa Muammar Gaddafi kwa utashi wao.

Mwaka mmoja uliopita kundi lijiitalo Dola la Kiislamu (IS) lilichukua udhibiti wa mji Sirte ambao ni makao ya kiongozi huyo wa zamani wa Libya, huku wakiendelea kufaidi kutokana na machafuko yaliotokea baada ya kifo chake mwaka 2011.

Mpasuko unaoendelea kukua kati ya Urusi na mataifa ya Magharibi uliochangiwa na mzozo mbaya wa mwaka 2014 nchini Ukraine.

Umeliacha Baraza la Usalama la UN kwenye mkwamo katika juhudi za kuleta amani Syria, ambako Urusi inaunga mkono Serikali ya Rais Bashar al-Assad huku Magharibi wakiunga mkono waasi wenye msimamo wa wastani.

Vita vya Syria vilianza mwaka 2011 kama maandamano ya kupinga utawala wa miongo minne wa familia ya Assad uliochochewa na machafuko yaliyoshuhudiwa katika mataifa ya Kiarabu kote Mashariki ya Kati.

Mataifa ya Magharibi yanasema Serikali ya Syria na mshirika wake Urusi yanakabiliwa na tuhuma za uhalifu wa kivita kwa kuwalenga raia, misaada ya kiutu na hata hospitali.

Hata hivyo, mataifa hayo mawili yamekanusha madai hayo na kusema mashambulizi yao yanawalenga tu wapiganaji.

Baada ya kushindikikana makubaliano mawili ya kusitisha vita mji wa Aleppo kati ya Marekani na Urusi, duru mpya ya mazungumzo imepangwa mjini Geneva, Uswisi mwezi huu, na itajumuisha mataifa ya Saudi Arabia na Qatar ambayo yanaunga mkono makundi ya upinzani nchini Syria.

Mgogoro wa Syria unaotoa sura ya jinsi migogoro duniani imekuwa migumu kutatulika kutokana na maslahi ya kila upande sawa na ambavyo Ufarasa ilikuwa na upande wake nchini Rwanda.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles