24.2 C
Dar es Salaam
Sunday, April 14, 2024

Contact us: [email protected]

SIDO YADHAMIRIA KUWAINUA WANANCHI KIUCHUMI

Na Mwandishi Wetu-Geita


SHIRIKA la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO), limejikita kusaidia kumwinua mwananchi mmoja mmoja kuondokana na umasikini kupitia viwanda kwa kusambaza ofisi zake nchi nzima.

Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, katika ziara yake ya kukagua maendeleo mkoani Geita.

“Nimefurahishwa na mwitikio wa wananchi katika maeneo yote niliyotembelea, SIDO inatoa teknolojia, mafunzo ya biashara, mikopo na masoko kwa wajasiriamali katika ofisi zake zilizosambaa mikoa yote nchini,” alisema Mwijage.

Baada ya kukabidhi eneo la kujenga ofisi za SIDO kwa mkandarasi mkoani hapa, Mwijage alisema SIDO inamjenga mtu kutoka kutojua kitu kabisa na kufikia hatua ya kusimama na kuanzisha mradi au kiwanda na kumfanya maisha yake kubadilika.

“Ili kufikia uchumi wa kati na viwanda 2025 ni lazima kubeba dhana ya uchumi wa viwanda jumuishi ambao hautamwacha Mtanzania yeyote nyuma, kwani kila mmoja atawajibika kwa nafasi yake hasa katika uanzishwaji wa viwanda vidogo,” alisema Mwijage.

Alisema ujenzi wa mabanda ya viwanda utasaidia kuwaunganisha wajasiriamali sehemu moja chini ya uangalizi wa SIDO utapelekea uzalishaji wa bidhaa kuwa bora na kupelekea ushindani sokoni.

Aidha, katika ujenzi wa mabanda hayo ya viwanda kutakuwa na chumba maalumu kwa ajili ya kuchakata vyakula na pia chumba cha baridi kwa ajili ya kuhifadhi bidhaa zisiharibike.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Robert Gabriel, alisema mkoa wake umejipanga kuwahamasisha wananchi kutembelea ofisi za SIDO ili wakajipatie mafunzo ya biashara na teknolojia itakayowasaidia katika kuanzisha na kuendeleza miradi yao.

“Geita inafursa za biashara, kilimo, migodi, hivyo wananchi wachangamkie fursa ili wajikwamue kiuchumi,” alisema Gabriel.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles