Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
MKUTANO wa Mtaa wa Temboni, Manispaa ya Ubungo Dar es Salaam, ambao ulikuwa ukijadili ufisadi katika mradi wa maji juzi, ulikumbwa na vurugu, huku watendaji na viongozi waliokuwa meza kuu wakisukumwa kwa kufanya uamuzi siasa.
Pamoja na wananchi, mkutano huo pia ulihudhuriwa na viongozi wa kata akiwamo Diwani wa Kata ya Msigani, Esrael Mushi (Chadema) na ofisa mtendaji wa kata hiyo.
Wananchi kwa kauli moja walikataa kamati ya maji isiendelee kuwapo baada ya kuwasilishwa ripoti ya Kamati ya Kikosikazi ambayo ilionyesha kuwa zaidi ya Sh milioni 2o zimetafunwa.
Akiwasilisha taarifa hiyo, Katibu wa Kamati ya Kikosikazi, Edmund Lusese, alisema kwa kipindi cha mwezi mmoja cha uchunguzi wa suala hilo, ilibainika baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Maji kwa kushirikiana na viongozi wa mtaa, walikuwa wakikusanya fedha na kuzitumia bila utaratibu.
Lusese aliomba mkutano huo kukubaliana kwa kauli moja kufanyika kwa uchunguzi huru ikiwamo kuletwa mkaguzi wa ndani wa hesabu wa Manispaa wa Ubungo ili kupata ukweli wa kile alichodai wizi wa fedha za umma katika mradi huo.
“Kwa mwezi mmoja yapo mengi tumeyabaini ikiwamo ukosefu na udhibiti wa fedha za maji, wapo baadhi ya wajumbe walikuwa wakiuza maji na fedha wanachukua wao binafsi lakini pia hata baadhi ya malipo yalikuwa yakifanyika bila kuwa na utaratibu ikiwamo ukosefu wa stakabadhi.
“Yote hii inatisha shaka na hata tumebaini kuwa zaidi ya Sh milioni 20 zimepotea kwa kipindi cha mwaka mmoja. Kwa hali hiyo tunawaomba wananchi muamue kwa busara kuhusu hali hii kwa sababu tunalia ukosefu wa maji kwa wetu wengi ila wapo wachache wanaonufaika na hali hii,” alisema Lusese.
Baada ya katibu huyo wa Kikosi kazi kumaliza kutoa maelezo hayo, Mwenyekiti wa Mtaa aliwahoji wananchi ambao kwa kauli moja waliazimia kamati ya maji ivunjwe na mradi huo wakabidhiwe Dawasco ili tija ipatikane.
Hata hivyo Diwani Mushi alisimama na kuomba kamati hiyo iendelee huku akiwaomba radhi wajumbe wa mkutano kutokana na makosa yaliyofanywa na wajumbe wa kamati.
Hata hivyo wananchi walikataa na wakaanza kuchagua wajumbe wapya wa kamati lakini wakiwa katika hatua za mwisho za kuwapigia kura wajumbe waliopendekezwa, alisimama Mhandisi wa Maji wa Manispaa ya Ubungo na kusema kuwa kama kuna viongozi wa siasa hawatakiwi kuwa wajumbe.
Maelekezo hayo yalipingwa na wananchi ambao walihoji kwa nini mhandisi huyo wa maji hakuyatoa mawazo kabla ya kuanza kupiga kura hali iliyozua vurugu na mkutano huo ukavunjika.
Mmoja wa wananchi kwenye mkutano huo aliyejitambulisha kwa jina la Sauda Mohamed, alisema suala la adha ya maji limekuwa likiwatesa hasa wananchi na kutokana na ufujaji wa fedha unaofanywa na baadhi ya wajumbe wa kamati ya maji.
Aliomba Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Humphrey Polepole na Wazari wa Maji na Umwagiliaji, Gerson Lwenge kuingilia kati mradi huo ukabidhiwe Dawasco.