NA EVANS MAGEGE,
WAKATI majaji 14 walioteuliwa kuendesha Divisheni ya Mahakama ya Rushwa na Ufisadi ya Mahakama Kuu wakitarajiwa kuanza mafunzo maalumu ya utendaji kazi wiki ijayo, Jaji mstaafu Amiri Manento, ameonya siasa kutoingilia mwenendo wa mahakama hiyo.
Jaji Manento alitoa onyo hilo jana jijini Dar es Salaam katika mahojiano maalumu na MTANZANIA Jumamosi lililotaka maoni yake kuhusu sifa wanazopaswa kuwa nazo watendaji katika mahakama ya mafisadi.
Akijibu swali hilo alisema inapaswa kufahamika kwanza kuwa lengo la kuanzishwa kwa mahakama hiyo ni kuharakisha kesi na si kubatilisha haki ya mtu.
“Lengo la kuanzishwa kwa mahakama hii ni ku- ‘accelerate’ (kuharakisha kesi) lakini si kubatilisha mambo kwamba haki ionekane batili au batili ionekane haki,” alisema Jaji Manento.
Alisema pamoja na lengo zuri la kuanzisha Divisheni ya Mahakama ya Rushwa na Ufisadi zipo dalili za uwapo wa kauli za kisiasa zinazoashiria kuingilia utendaji wa mahakama hiyo kwa namna moja au nyingine.
Akizungumzia kile kinachoigusa jamii tangu ilipotangazwa nia ya kuanzishwa kwa mahakama hiyo, Jaji Manento ambaye amewahi kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, alisema watu wengi wamekuwa wakiufuatilia katika mtazamo wa kisiasa.
“Watu wanafuatilia vitu kisiasa. Pia ni sahihi kwamba majaji 14 wameteuliwa kuongoza mahakama hii lakini inategemea kesi ngapi zitafikishwa maana lazima watu washtakiwe na Jamhuri.
“Kwa mfano leo Jamhuri inaleta kesi 14 wakasema ushahidi umekamilika na majaji wakapangiana kila mtu mmoja mmoja, kesho tena wakaletwa 14 kwa hiyo kila siku wanaleta, swali la kujiuliza hao mashahidi wamewaleta wote?
“Au, unakuta shahidi yupo Marekani sasa ni mpaka arudi kwa hiyo huyu Jaji itabidi aiahirishe kesi mpaka Serikali ilete mashahidi wake, vivyo hivyo katika kujitetea mtuhumiwa naye anasema kuwa shahidi wake yupo kwenye matibabu India labda baada ya wiki sita atarudi. Ndiyo maana nasema kuwapo ‘political statement’, maana kama Jaji hutaweza kutoa hukumu bila kusikiliza pande zote mbili,” alisema Jaji Manento.
Aidha, gwiji huyo wa sheria alisema uharaka wa hukumu dhidi ya watuhumiwa watakaofikishwa mahakamani utatokana na kukamilika mapema kwa ushahidi na kwamba upo uwezekano wa kesi kusikilizwa hadi saa 12 jioni.
“Lakini Serikali wakiharakisha kwa mfano mtuhumiwa kasomewa mashtaka leo na amekana, wakasema tunaomba tarehe ya kusikilizwa tena Jaji akasema kesho na kesho wakaletwa mashahidi wote, uzoefu wangu unaonyesha kwamba ni vigumu sana kwa Jaji kuahirisha kesi kama mashahidi wapo, kesi itasikilizwa mpaka saa 12 na iendelee kesho yake.
“Hapo hakimu baada ya kusikiliza mashahidi wa upande mmoja atageukia upande mwingine na kwa ujumla kesi ambayo imeleta mashahidi kwa haraka hata hukumu inatoka kwa haraka kwa sababu kila kitu kipo kichwani, lakini ikichelewa sana utakuwa umesahau kwa sababu unapoandika hukumu unamuona yule shahidi usoni mwako jinsi alivyokuwa anaongea kwa sababu utamsoma kwa jinsi alivyokuwa anazungumza,” alisema Jaji Manento.
Alisema uamuzi wa Serikali kuwapa majaji na mahakimu muda wa miezi tisa kutoa hukumu kwa kesi zilizokamilisha ushahidi utasaidia kuwabana ambao ni wavivu.
“Muda wa miezi tisa unatosha kutoa hukumu kwa kesi ambayo imekamilisha ushahidi, lakini kuna ‘forces’ hapa ya ndani kwa sababu Jaji anaweza kufikia uamuzi wa kuifuta kesi.
“Kama akiifuta kuna vifungu viwili kimoja kinasema ukiifuta ni kama imekwisha moja kwa moja na mtuhumiwa hutashitakiwa tena kwa kosa hilo na kifungu kingine kinasema tunaifuta lakini mtakapokamilisha taratibu zetu tutamfungulia tena kwa kosa hilo hilo,” alifafanua Jaji Manento.
Akizungumzia aina za utendaji kazi wa majaji wawapo kazini au katika maisha binafsi alisema uzoefu wake unawaweka katika makundi matatu.
Akiyataja makundi hayo alisema la kwanza ni la wale ambao ni wepesi kutoa hukumu na pili la wavivu na mwisho ni majaji ambao hufanya utafiti kabla ya kuhukumu hivyo kujikuta wakichelewa kutoa hukumu.
“Nimeeleza vitu vitatu, nimesema unaweza ukaiandika hukumu haraka na kutoa majibu kuwa aliyeshindwa ameshindwa na kila kitu kipo pale na huyu mtu mwingine hukumu ile ile akaifanyia research na hii inaweza kufundishia hata chuo kikuu, wa tatu ni mvivu sasa kuna justice deride na justice dinnared.
“Kuna majaji ambao ni ‘fast’ ukichukulia misemo ya kisheria isemayo ‘Justice delayed, justice denied’ alafu kuna Justice hurried, justice buried hapa utakuta kuna mchanganyiko mkubwa.
“Kuna watu kama Jaji aidha ni mvivu sana, anapenda kuongea lakini ni mvivu tu, mwingine anaweza akachelewesha kidogo lakini anafanya utafiti wa kina sana ambao ukiusoma unaona kazi imefanyika hata kama imechelewa.
“Lakini mwingine anaandika haraka haraka bila kufanya utafiti anakwenda moja kwa moja kwenye lengo na pointi zake ukisoma utabaini hukumu imefanyika, lakini hauwezi kuitumia kufundishia chuo kikuu,” alisema Jaji Manento.