28.7 C
Dar es Salaam
Thursday, June 13, 2024

Contact us: [email protected]

Shule ya Sekondari Bwawani yaanza kudhibiti vitendo vya ushoga, usagaji

Na Ashura Kazinja, Morogoro.

Shule ya Sekondari ya Bwawani imeanza kutoa elimu ya ukakamavu kwa wanafunzi wake ili kuwajengea uwezo wa kujilinda na kukabiliana na vitendo ukatili ikiwamo kujiingiza katika mapenzi ya jinsia moja.

Mgeni Rasmi na Kamishina Jenerali wa Magereza, Afande Mzee Ramadhani Nyamka (aliyevaa skafu) akizindua jengo la Utawala katika shule ya sekondari Bwawani.

Hayo yamebainishwa Aprili 26, 2023 na Mkuu wa shule hiyo, Anthony Sogoseye (ACP) katika mahafali ya nane ya kidato cha sita yaliyofanyika shuleni hapo ambapo amesema mafunzo hayo yakiwemo ya kareti yatawasaidia wanafunzi hao katika kuimarisha afya zao, mwili, kiakili pamoja na kujilinda dhidi ya vitendo viovu ikiwemo kupambana na ushoga na usagaji.

Sogoseye amesema mbali na shule hiyo kuwa taasisi ya kutoa taaluma pia wanatoa mafunzo ya ukakamavu na skauti ili kuwajengea wanafunzi uzalendo na wenye mapenzi mema kwa taifa lao pamoja na kuwa tayari kuwahudumia watu wengine bila ubaguzi.

“Shule kama Taasisi ya taaluma hatujihusishi na taaluma peke yake bali tunafanya mambo mengine kama mafunzo ya ukakamavu na skauti, wanafunzi wanapata fursa ya kushiriki na kujifunza mafunzo ya gwaride kwa ajili wa kuwajenga kuwa wakakamavu na wengine wachache wamejisajili kuwa skauti na mafunzo hayo yanawakuza katika uzalendo na mapenzi mema kwa taifa letu,” amesema ACP Sogoseye.

Aidha, amesema kukamilika kwa ujenzi wa jengo la utawala, ukumbi wa mikutano na sherehe pamoja na fremu za biashara kumeboresha mazingira ya utendaji kazi kwa watumishi wote shuleni hapo na kwamba wanatarajia kuendelea na ukarabati wa mabweni, ujenzi wa nyumba za watumishi na kuendeleza ujenzi wa ukuta kuzunguka shule kadri fedha itakavyokuwa inapatikana.

Wanafunzi kidato cha sita Shule ya Sekondari Bwawani wakiwa katika picha ya pamoja na uongozi wa shule hiyo pamoja na mgeni rasmi.

Akizungumza kwa niaba ya wazazi, Fanuel Aidani, ameushukuru uongozi wa shule hiyo kwa malezi mema inayowapa watoto wao ikiwemo kupinga vikali vitendo vya ushoga na usagaji, huku akiwaasa wanafunzi hao kukaa mbali na uovu, kutobweteka na kusoma kwa bidii ili waweze kufanya vizuri katika mitihani yao na maisha kwa ujumla.

Wakisoma Risala kwa Mgeni rasmi wanafunzi kidato cha sita, Sheshi Athumani na Lowasa State, wameushukuru uongozi wa shule hiyo kwa elimu bora inayowapatia, malezi pamoja na huduma mbalimbali kama chakula, malazi, mavazi na huduma ya kiroho.

Pia wameuomba uongozi wa shule hiyo kutatua changamoto ya upungufu wa wahudumu katika zahanati ya shule na udogo wa bwalo la kulia chakula wanafunzi, kutokana na idadi ya wanafunzi kuendelea kuongezeka.

Kwa upande wake Kamishina Jenerali wa Magereza Afande Mzee Ramadhani Nyamka, amewataka wazazi na walezi wa wanafunzi kuendelea kuwalea vyema pindi wakirudi nyumbani na kuhakikisha kuwa hawaingii katika mambo yasiyofaa yanayozidi kuibuka kila siku ikikiwemo ndoa za jinsia moja, matumizi ya madawa ya kulevya pamoja na mmomonyoko wa maadili kwa ujumla.

“Naomba tuendelee kuwalea vyema na kuhakikisha kuwa hawaingii katika mambo yasiyofaa yanayozidi kuibuka kila uchao, mfano kutumia madawa ya kulevya na kuathiri ndoto zao na zenu za kusoma mpaka chuo kikuu na kuhakikisha wanakuwa wa manufaa kwao wenyewe na familia na taifa kwa ujumla,” amesema Nyamka na kuongeza kuwa:

“Hivi sasa tumeshuhudia vitendo vya mmomonyoko wa maadili kila kukicha unasikia mambo ya ndoa za jinsia moja, na ninashukuru kwamba vijana hapa wametuambia ndoa za jinsia moja hazikubaliki ni kinyume cha utamaduni, mila, desturi na hulka za kiafrika, kama vitendo hivyo ndio tunaambiwa ni mabadiliko ya sayansi na teknolojia, ndio haki za kibinadamu, kwa sisi waafrika ambao tumerithi mila zetu toka kwa mababu zetu kitu hiki hakikubaliki.

“Nchi hii inahitaji watu au kizazi ambacho kitarithi nchi hii baada ya sisi kuondoka, ndio watakuwa walinzi wa taifa hili, tunatarajia kutoa wanajeshi humu, polisi magereza, madaktari,wachumi, wafanyabiashara  na wengineo, sasa kwenye jamii ya ndoa ya jinsia moja hao warithi watatokea wapi, mwisho itafika mahali nchi hii itakuwa haina mwenyewe, ndio ukoloni utarudi tena kwa njia nyingine, tutakuwa hatuna askari wa kulinda nchi, itabidi waje kutusaidia kuilinda na ndiyo itakuwa tayari wameshaichukua, wakisharudi kwa njia hiyo ukoloni huo itakuwa ngumu kuuondoa, hivyo tuukatae kwa dhati kabisa kwamba Tanzania hii haina nafasi ya ushoga na wasagaji,” amesisitiza.

Pia amewaasa wahitimu wa kike kuwaogopa kama ukoma na kuwa nao makini  mafataki ambao ni wanaume wanaopenda kuwadanganya mabinti wadogo, kwani watawafanyia kila hila na mbinu ikiwemo mitego mbalimbali ili kuwaharibia maisha yao ya baadae.

Shule hiyo inayomilikiwa na Jeshi la Magereza nchini iliyopo mkoani Pwani katika wilaya ya Chalinze, ni miongoni mwa shule chache zinazofanya vizuri kitaaluma, michezo na hata katika malezi ikiwa ni pamoja na kuwafundisha wanafunzi wake ujasiriamali mbalimbali utakaowasaidia katika maisha yao ya baadae, jumla ya wanafuzi 35, wavulana 21 na wasichana 14 wanatarajiwa kuhitimu kidato cha sita mwezi mei mwaka huu.  

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles