25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Shule tano za msingi zaongoza kwa ulawiti

Waziri Nashiri
Waziri Nashiri

Na Patricia Kimelemeta, Dar es Salaam

SHULE ya Msingi Kimanga na Tumaini za Ilala, Dar es Salaam, zinaongoza kwa vitendo vya wanafunzi kulawitiana hali inayosababisha kutofanya vizuri darasani.

Hayo yalisemwa na Ofisa Kiongozi wa Ustawi wa Jamii Manispaa ya Ilala, Waziri Nashiri wakati wa mkutano na wadau wa mabadiliko uliofanyika Dar es Salaam jana.

Alisema tathimini iliyofanywa kuanzia Januari hadi Juni mwaka huu, ilibaini kuwa shule hizo na  nyingine tatu ambazo wanafunzi wamepata matatizo hayo.

Shule nyingine ni Shule ya Msingi Tabata, Magoza iliyopo Kinyerezi na Shule ya Msingi Kisukuru.

Nashiri alisema watoto hao wamekuwa wakifanyiana vitendo hivyo wenyewe kwa wenyewe hali iliyosababisha wanafunzi wengine kujiingiza kwenye mkumbo huo.

“Ni zaidi ya shule tano za Manispaa ya Ilala wanafunzi wake wameathirika na vitendo vya kulawitiwa, hali iliyosababisha idadi kubwa ya wanafunzi kushindwa kufanya vizuri kwenye masomo yao darasani.

“Katika tathmini hiyo, tumebaini kuwa idadi kubwa ya wanafunzi hao wameanza kufanya vitendo hivyo na ndugu na jamaa zao, hali iliyosababisha kwenda kuwashawishi wanafunzi wenzao shuleni na kuanza kuingiliana wenyewe kwa wenyewe,” alisema Nashiri.

Alisema pia wameweza kubaini kuwa kati ya watoto 10, watoto wa kiume wanne wamelawitiwa na ndugu, jamaa au wanafunzi wenzao, huku watoto wa kike wanne wamebakwa huenda na ndugu zao au baba walezi.

Pamoja na mambo mengine, Nashiri alisema kuongezeka kwa tatizo hilo kunatokana na baadhi ya wazazi kushindwa kutoa ushirikiano baada ya watoto wao kubainika kufanyiwa vitendo hivyo, jambo ambalo limechangia kuendelea kufanyika kwa vitendo hivyo.

“Tumewasiliana na walimu wakuu wa shule hizo pamoja na wazazi wao kwa ajili ya kujadili jambo hilo na kutafuta njia mbadala ya kuwanasua wanafunzi ambao bado hawajafanyiwa vitendo hivyo.

“Tumeanzisha programu yetu inaitwa ‘mkono kwa mkono’ ipo Amana. Watendaji wake wanazunguka kila sehemu katika manispaa yetu kwa ajili ya kuongea na wazazi juu ya kukithiri kwa vitendo vya ukatili ikiwamo ulawiti, lengo ni kupunguza ukubwa wa tatizo hilo,” alisema.

Aidha, alisema hadi sasa manispaa hiyo pia imeweza kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwamo wana mabadiliko kuhakikisha kuwa wanatoa elimu kwa wazazi ili waweze kutambua kuwa ukatili ni tatizo kubwa na kwamba linapaswa kupigwa vita na kila mmoja katika jamii inayowazunguka.

Alisema changamoto wanayokutana nayo ni baadhi ya wazazi kushindwa kutoa ushirikiano mara baada ya kubaini kuwa tatizo hilo limeanzia ndani ya familia.

“Wazazi wengi wanashindwa kutoa ushirikiano pindi wanapoona watoto wameanza kulawitiwa na ndugu ama jamaa, tena wengi wao ndiyo wanakuwa mstari wa mbele kwenda kuwawekea dhamana pale tunapowafikisha polisi au mahakamani kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria,” alisema.

Mkurugenzi wa Kituo cha Msaada wa Kisheria kwa Wanawake (WLAC),Theodosia Muhulo, alisema kuwa vitendo vya ukatili ni tatizo kubwa nchi nzima, jambo ambalo limechangia wanawake wengi kukata tamaa ya maisha.

“Tumezunguka mikoa mbalimbali nchini kwa ajili ya kufanya tathimini ya vitendo vya ukatili, lakini tumebaini tatizo hilo ni kubwa ambalo linahitaji ushirikishwaji wa kila mmoja wetu katika jamii inayotuzunguka,” alisema Muhulo.

Alisema mkakati uliopo ni kuendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha kuwa wanatoa elimu kwa wananchi ili waweze kutambua athari ya ukatili na jinsi ya kuripoti pale wanapoona kumetokea vitendo kama hivyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles