23.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

MCT yalaani ukandamizaji vyombo vya habari

Kajubi Mukajanga.
Kajubi Mukajanga.

Na Veronica Romwald, Dar es Salaam

BARAZA la Habari Tanzania (MCT) limelaani ukandamizaji wa uhuru wa habari unaofanywa na serikali kwa kufungua vyombo vya habari kila inapojisikia kufanya hivyo.

Akizungumza katika mkutano wa 18 wa wanachama wa MCT   Dar es Salaam jana, Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Kajubi Mukajanga alisema inasikitisha kuona bado kuna uminyaji wa uhuru wa habari nchini.

“Tangu mwaka huu uanze kumekuwa na ukandamizaji wa uhuru wa vyombo vya habari na haki ya kupata habari kwa ujumla.

“MCT tunasikitika kuona kwamba sheria ambazo tumekuwa tukizilalamikia ndizo zinazotumika wakati huu tena kwa wingi kuliko wakati mwingine wowote ule.

“Sheria ambazo tumeshasema hazifai tangu wakati wa Nyalali hasa ile ya magazeti ya mwaka 1976 na Waziri mwenye dhamana na masuala ya habari alikiri kuwa zina matatizo na akasema lazima zibadilishwe.

“Tunasikitika kwa nini zinatumika  hivi sasa wakati tupo kwenye mchakato wa kuzibadili,” alisema Mukajanga.

Alisema MCT inaipongeza Serikali kwa kupambana na rushwa lakini vyombo vya habari vina nafasi  muhimu katika vita hiyo.

“Vyombo vya habari ni rafiki katika mapambano ya vita hivyo katika kufichua maovu na wala rushwa ili Serikali ichukue hatua, lakini kunapokuwa na uminyaji wa uhuru wa habari vita hiyo inakuwa ngumu,” alisema.

Alisema MCT inapitia taarifa ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye ya kulifungia gazeti la Mseto na ile ya Redio 5 na Magic kuona ni namna gani vyombo hivyo vimeingia kwenye mgogoro na serikali.

“Kamati baada ya kumaliza kazi ya kupitia taarifa hiyo tutakwenda kuonana na Waziri Nape. Na kuanzia katika bajeti yetu ijayo tuna mpango mkakati wa kuweka kipengele cha kusaidia uhuru wa habari kwa kuwezesha kesi ambazo zitakuwa zikifunguliwa mahakamani na katika hili tumeanza na kesi iliyofunguliwa na Jamii Forum,” alisema.

Awali, akichangia mada katika mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mwanahalisi, Saed Kubenea aliiomba MCT iwe inasaidia kwa namna moja au nyingine   mmiliki au mwanahabari anapofungua kesi mahakamani.

“Nasema hivi kwa sababu gharama za uendeshaji wa kesi ni kubwa na mara nyingi zinachukua muda mrefu.

“Ni vema MCT mkasaidia katika usimamizi wa kesi hizi kwa sababu nguvu ya mtu mmoja mmoja ni ndogo lakini MCT ikiwapo itaongeza nguvu ya madai,” alisema.

Mwenyekiti wa Bodi ya MCT, Jaji Thomas Mihayo alikubaliana na wazo hilo huku akimpongeza mwanahabari huyo ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo kwa kushinda kesi yake iliyosababisha  kufunguliwa kwa gazeti la Mwanahalisi.

“Tumeelezwa kuwa katika kipindi cha 2015 wanahabari walipatwa na madhira mbalimbali ikiwamo kupigwa, kuharibiwa vifaa vyao ikiwa ni sawa na asilimia 75 na yote yalihusishwa na Uchaguzi Mkuu.

“Nawashauri wanahabari inapofika kudai haki, msisinyae na kusubiri wengine wawasemee… nendeni mahakamani huko ndiko ambako haki inaweza kupatikana,” alishauri.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles