25.3 C
Dar es Salaam
Friday, January 3, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Shoo fainali ya Championi wa Kitaa ilivyoacha gumzo Dar

NA WINFRIDA MTOI, Mtanzania Digital

PAMBANO la masumbwi la fainali ya Championi wa Kitaa, imeacha gumzo kwa mashabiki wa mchezo huo kutokana na ushindani mkubwa wa mabondia, huku vipaji vipya vikidhihirisha ubora wao ulingo wa ndondi.

Fainali hiyo iliyomalizika usiku wa kuamkia leo Machi 21, 2022 kwenye Uwanja wa Ndani wa Taifa, ilivuta mashabiki wengi kutoka maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam.

Uwepo wa mashabiki hao ambao kila mmoja alikuwa anasapoti mabondia wake, pamoja na wadau tofauti wa mchezo huo ikiwamo mabondia wa zamani kuliifanya fainali hiyo kuwa ya kipekee.

Mwamuzi Chaurembo Palasa akimhesabia Hassan Ndoga kama anaweza kuendelea na pambano baada ya kuangushwa na na mpinzani wake Mbega.

Mashindano hayo ya Championi wa Kitaa yaliyoandaliwa kwa mara ya kwanza mwaka huu na kampuni ya Peaktime Media yakianzia Wilaya ya Temeke, lengo lake ni kuinua vipaji vya ngumi kuanzia ngazi ya chini na kuviendeleza.

Michuano hiyo ilizinduliwa Februari 13,2022 Tandika jijini Dar es Salaam kwa mabondia mbalimbali kuzichapa ambapo washindi walikutana nusu fainali iliyopigwa Februari 20,2022 kwenye Ukumbi wa Zakhiem, Mbagala.

Dullah Mbabe (kulia), akipambana na Amour Haji jana katika fainali ya Champion wa Kitaa kwenye Uwanja wa Ndani wa Taifa, Dar es Salaam
Amour Haji akiwa chini baada ya kuangushwa na ngumi nzito ya Dulla Mbabe katika raundi ya pili ya pambano

Mabondia walioibuka kidedea ndiyo waliozichapa jana, huku wakisindikizwa na wanamasumbwi wengine walionogesha mpambano huo akiwamo bondia maarufu Abdallah Pazi ‘Dulla Mbabe’ ambaye alimchapa Amour Haji kwa K.O raundi ya pili.

Pambano la Dulla Mbabe na Haji lilikuwa la raundi sita uzito wa kilo 76 ambapo mabondia hao walikutana kwa mara ya pili na Dulla kuendeleza ubabe kwa mpinzani wake.
Dulla Mbabe amesema pambano hilo amelitumia kujipima na kuwapa zawadi mashabiki, kwani kocha wake Habib Kinyogori alimuambia akajaribu mitambo kama yuko fiti.

“Niko salama, mashabiki wa Dulla wakae mkao wa kula, tutaandaa pambano kubwa na mashabiki mtanipenda na mtaendelea kumpenda. Mimi ndio bondia pekee Afrika niliyepiga watu K.O mara 30 na nilimeleta mkanda wa dunia nchini,’ametamba Dulla.

Ally Ngwando (kulia) bingwa wa PST akichapana na James Kibazange

Pambano lingine lililokuwa la msisimko raundi nane kilo 51, liliwakutanisha mabondia vijana wenye upinzani wa hali ya juu, Ally Ngwando dhidi ya James Kibazange na Ngwando kuibuka kidedea na kutwaa ubingwa wa PST.

Naye Hassan Ndonga maarufu Tyson wa Bongo, alishindwa kufurukuta baada ya kuchezea kichapo cha T.K.O kutoka kwa Adam Mbega, akiangushwa chini mara tano katika mchezo uliokuwa wa raundi nane kilo 55.

Kipigo cha Ndonga kiliiwaacha na simanzi mashabiki wake waliojaa ukumbini hapo kutokana na kushindwa kuamini kile kilichokuwa kinatokea kwa bondia wao aliyekuwa na historia nzuri katika mapambano yake yaliyopita.

Promota Meja Seleman Semunyu akimvalisha mkanda wa ubingwa wa PST, Ally Ngwando baada ya kuibuka bingwa.

Bondia mwingine aliyewavutia mashabiki ni Said Mkola aliyeingia na staili ya tofauti ulingoni kwa kuonyesha vionjo mbalimbali vya kucheza huku akiwa anapigana na kufanikiwa kuibuka mshindi kwa K.O dhidi ya Hamad Mkude.

Moja ya staili ya mkola iliyowafanya mashabiki waliofurika uwanja wa ndani kupiga kelele za shangwe ni kitendo cha kucheza mtindo maarufu wa kutetema wa straika wa Yanga, Fiston Mayele anapofunga bao.

“Mashabiki zangu naomba waendelee kunipa sapoti, nawaahidi kuendelea kufanya vizuri kwa sababu sapoti niliyoiona hapa ilinifanya nifurahi. Kauli mbiu yangu ni ile ile ya Piga Jitu Uwa Jitu. Kwa sasa kati ya mabondia ninaowataka kupigana nao ni Baina Mazola,” ametamba Mkola.

Seleman Galile akitangazwa mshindi na mwamuzi Anthony Rutta baada ya kumchapa Mussa Dragon

Kwa upande wa Hassan Kube hali haikuwa nzuri kwake baada kuangukia kisogo na kupoteza kumbukumbu kutokana na ngumi kali ya Max Mushi na kumfanya akimbizwe hospitali.

Naye Mussa Dragon ambaye ametokea katika mchezo wa ‘Kick Boxing’ ameonekana bado kwenye ndondi hajakolea baada ya kushindwa kuendelea na pambano katika raundi ya tano na kumfanya mpinzani wake Seleman Galile kuibuka mshindi.

Katika pambano kuu la Champion wa Kitaa, Moano Ally kutoka Bagamoyo aliibuka kinara dhidi ya Salehe Mkalekwa, mchezo uliokuwa wa raundi nane kilo 76.

Mapambano mengine Swahibu Ramadhani amemchapa Said, Uwezo, huku Vigulo Shafii akiambulia kichapo kutoka kwa Hemed Rashidi na Omary Mpemba akimtwanga K.O Mahmoud Omary.

Hussein Mkalekwa(kushoto), akionyeshana kazi na Jadi Salehe

Matokeo mengine Muhidin Kavinga amempiga Uwesu Mbetu, Omary Bakari alipigwa K.O na Bonny Sela, Hussein Mkalekwa alishinda dhidi ya Jadi Salehe, huku Peter Tosh akitoka sare na Maneno Osward JR na Shaban Kimimbi alimchapa Abdallah Muhumba.

Neno la Promota

Akizungumzia mchuano huo, Promota muandaaji wa Champion wa Kitaa kutoka Peaktime Media, Meja Selemani Semunyu, amesema kutokana na sapoti ya mashabiki waliojitokeza kushuhudia fainali hiyo, inaonesha jinsi gani walivyoipokea michuano hiyo vizuri.

Amesema amefarijika kuona vipaji vipya viliivyonesha uwezo na upinzani wa hali ya juu na kuahidi kuviendeleza vipaji hivyo kwa kuvijumuisha katika mapambano makubwa, huku akiendelea kuibua wengine.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles