Brighiter Masaki -Dar es salaam
NAIBU Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Juliana Shonza, amewataka wasanii kujisajili katika Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) ili kuweza kupata fursa zilizopo ndani na nje ya Tanzania kwa kutumia vipaji vyao.
Akizungumza na MTANZANIA mwishoni mwa wiki iliopita mara baada ya ufunguzi wa duka la mbunifu wa mavazi Ally Rehmtullah, linalowasaidia wabunifu wasio na ofisi kutengeneza na kuuza nguo zao, Shonza alisema msanii unapojisajili Baraza linamsaidia zinapotokea fursa ya kufanya kazi nje na ndani kupata kibali kwa haraka.
“Wasanii wengi wamekuwa wakilalamika kuwa wananyimwa na kukosa fursa hata zinapotokea, wanakosa kibali cha kwenda kufanya kazi zao nje, hii yote ni kutokana na kutotambulika, wakati mwingine hata fursa zinapotokea wanachukuliwa wachache,”alisema Shonza.
Aidha aliongeza kuwa anampongeza Rehmtulla kwa kuweza kiwafikiria wabunifu wenzake na kuweza kuwasaidia kuwapa nafasi wabunifu wengine kujitangaza.