Na Norah Damian, Mtanzania Digital
Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu (Shivyawata) limeiomba Serikali kuwasaka na kuwachukulia hatua watu wanaotaka viungo vya watu wenye ualbino ili kudhibiti mauaji ambayo yameanza kuibuka tena.
Novemba 2, mwaka huu mkazi wa Kijiji cha Ngula kilichopo Wilaya ya Kwimba jijini Mwanza, Joseph Mathias mwenye ualbino alivamiwa na wahalifu waliomkata mkono na kusababisha kifo chake.
Akizungumza na Mtanzania Digital, Mwenyekiti wa Shivyawata, Ernest Kimaya, amesema mara zote wamekuwa wakikamatwa watu waliotumwa kutafuta viungo vya watu wenye ualbino.
“Hatukuwahi kuishika mizizi (yaani wanaotaka viungo vya watu wenye ualbino), ila tumepunguza matawi, wale wanaotumwa kuua au kuwataka viungo ndugu zetu.
“Tunaiomba Serikali wadhibiti jambo hili kabla halijawa kubwa zaidi ili wenye ualbino waweze kuishi kwa amani,” amesema Kimaya.
Tayari Jeshi la Polisi limewakamata watu watano wakituhumiwa kuhusika na mauaji hayo.
Kwa miaka mitano kuanzia 2015 mpaka 2020 hakukuwa na ripoti yoyote ya mauaji dhidi ya watu wenye ualbino lakini Mei 2021, mkoani Tabora kulitokea mauaji ya mtoto mwenye ualbino ambapo mwili wake uliokotwa ukiwa umekatwa viungo mbalimbali ikiwamo mikono.
Aidha Novemba 2021 kulitokea tukio lingine wilayani Lushoto mkoani Tanga ambapo mwili wa Kheri Shekigenda aliyekuwa amezikwa katika makaburi wilayani humo ulifukuliwa na viungo vyake kuchukuliwa.
Pia Aprili 2022, liliripotiwa tukio lingine ambapo mkazi wa Mabibo Dar es Salaam, Mohamed Rajabu alivamiwa na kukatwa na panga na watu wasiojulikana.