24.2 C
Dar es Salaam
Monday, May 27, 2024

Contact us: [email protected]

Wenye ulemavu waona matumaini kukopa mmoja mmoja

Na Norah Damian, Mtanzania Digital

Baada ya Serikali kufanya marekebisho ya sheria yanayoruhusu watu wenye ulemavu kukopa mikopo inayotolewa na halmashauri bila kuwa kwenye kikundi, wengi wamechangamkia fursa hiyo.

Serikali imeelekeza kila halmashauri kutenga asilimia 10 ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya kuwawezesha wanawake, vijana na wenye ulemavu kwa kuwapatia mikopo isiyokuwa na riba.

Wakizungumza na Mtanzania Digital kwa nyakati tofauti baadhi ya wanufaika wa mikopo hiyo wamesema utaratibu huo umeondoa changamoto walizokuwa wakipata awali kwenye vikundi.

Mmoja wa wanufaika, Hashimu Hassan mwenye ulemavu wa viungo na mkazi wa Wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma, amesema amekopeshwa Sh milioni 3 zilizomwezesha kuongeza biashara ya mashine ya kusaga nafaka kutoka steshenari aliyokuwa nayo awali.

“Nilikopa Sh milioni tatu mpaka sasa bado Sh milioni moja nimalize deni nikope tena, biashara inakwenda vizuri,” amesema Hassan.

Hata hivyo ameiomba Serikali kuangalia upya muda wa urejeshaji mikopo hiyo ikiwezekana iongezwe hadi miaka mitatu kwa mikopo mikubwa.

Aidha katika Manispaa ya Mtwara kwa mwaka 2021,22 imefanikiwa kukopesha Sh milioni 26.7 kwa kikundi kimoja cha watu watano wenye ulemavu wakati mikopo ya mtu mmoja mmoja walikopeshwa watu saba.

Ofisa Maendeleo ya Jamii katika Manispaa ya Mtwara, John Samo, ameiambia Mtanzania Digital kuwa kwa mwaka wa 2022,23 wanatarajia kutoa mikopo yenye thamani ya Sh milioni 27.2 kwa watu saba wenye ulemavu.

Nalo Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu (Shivyawata) limesema kupitia mradi wa kuwajengea uwezo wanachama wake kuhusu masuala ya utunzaji fedha na elimu ya ujasiriamali wengi wamekuwa na mwamko wa kukopa na kujiendeleza kiuchumi.

Mratibu wa Mradi huo Wilaya ya Kondoa, Salama Salum, amesema umeleta tija kwani watu wengi sasa wanajitambua, wanaelewa namna ya kufanya biashara, kubuni miradi, kutunza kumbukumbu, kukopa na kurejesha kwa wakati.

Mradi huo unatekelezwa katika Halmashauri ya Jiji la Tanga na Korogwe (Tanga), Dodoma Mjini na Kondoa (Dodoma), Mwanza Mjini na Ilemela (Mwanza).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles