Na Mwandishi Wetu, Morogoro
Shirika la Social Action Fund (SATF) linalojihusisha na kuwawezesha kielimu watoto walio katika mazingira magumu limekabidhi vitendea kazi vyenye thamani ya Sh milioni 51 zikiwemo kompyuta 18, ili kuimarisha utendaji kazi.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo yaliyofanyika Mei 28, 2021, mjini Morogoro, Meneja miradi wa shirika hilo, Nelson Rugambwa amesema vifaa hivyo vitasaidia katika utunzaji wa taarifa.
“Tumekabidhi vifaa hivi ikiwa ni pamoja na kompyuta 18 na vifaa vya kuunganishia mtandao vyenye thamani ya Sh milioni 51 kwa wadau watekelezaji (implementing Partners).
“Vifaa hivi vitasaidia katika utunzaji wa taarifa na kurahisisha mawasiliano ya kati yao na shirika, kwani tumeona katika kuboresha huduma zetu tuwapatie vitendea kazi wadau wetu ili kuwaondolea changamoto mbalimbali zilizokuwa zilizokuwa zikiwakwamisha katika utendaji wa kazi wao.
“Kwa sasa kazi zitakuwa rahisi sana maana watakuwa na kanzi data ya kutunza taarifa za miradi yao pamoja na kuwa na mawasiliano ya mtandao ya moja kwa moja na wasimamizi wa SATF na kufanya mawasiliano pasipo kulazimika kukutana moja kwa moja,” amesema Rugambwa.
Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa (SATF), Beatrice Mgaya, mara baada ya kuwakabidhi wadau watekelezaji (implementing partners) kompyuta 18 na vifaa vya kuunganishia mtandao vyenye thamani ya Sh milioni 51 amewataka kufanya kazi kwa weledi na uaminifu.
“Tumetoa vifaa hivi kwa lengo la kurahisisha utendaji kazi, hivyo tufanye kazi kwa kujitolea ili kusadia jamii hasa watoto tuwawezeshe kupata elimu kutokana na changamoto zinazowakabili za ukatili, unyanyasaji, mazingira magumu na umasikini wa familia zao,” amesema.
Vifaa hivyo vimekabidhiwa kwa wawakilishi wa vituo mbalimbali hapa nchini.