21.5 C
Dar es Salaam
Saturday, July 27, 2024

Contact us: [email protected]

Shirika la JHPIEGO lawapiga msasa wanahabari kuhusu Afya ya Uzazi

Na Janeth Mushi, Arusha

Shirika lisilo la kiserikali la JHPIEGO kupitia mradi wa Tupange Pamoja (TCI), kwa kushirikiana na Idara ya Afya Mkoa wa Arusha, limetoa mafunzo kwa waandishi wa habari mkoani hapa kuhusiana na Afya ya Uzazi kwa Vijana.

Aidha, imeelezwa kuwa elimu ya kutosha ikitolewa kwa kundi vijana kuhusu afya ya uzazi,itasaidia kupunguza maambukizi ya Virusi vya Ukimwi, mimba katika umri mdogo pamoja na ndoa za utotoni.

Akizungumza jana wakati wa mafunzi hayo Mratibu wa Shirika hilo mkoani Arusha, Waziri Njau, amesema vyombo vya habari bado vina nafasi kubwa ya kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa afya ya uzazi kwa vijana kwani bado jamii hasa vijana haijawa na uelewa wa kutosha juu ya masuala ya afya ya uzazi.

“Ukiangalia katika jamii bado kundi la vijana wana changamoto kubwa,hata huduma rafiki kwa vijana bado jamii haijawa na uelewa nayo ndiyo maana tunataka nyie waandishi wa habari muwe na uelewa juu ya hili ili muweze kuelimisha jamii kwani mna jukwaa kubwa la kufanya hivyo.

Sehemu ya Washiriki

“Baadhi ya changamoto katika kundi hili ni pamoja na matumizi ya njia za kisasa za uzazi wa mpango kuwa chini kwa kundi la vijana pamoja na tatizo la vijana la afya ya akili linalosababishwa na matumizi ya dawa za kulevya,” amesema Njau.

Amesema kupitia mradi huo mbali na elimu katika makundi mbalimbali katika jamii pia wametoa elimu hiyo katika Vyuo mbalimbali ikiwemo cha Makumira,Uhasibu (IAA) pamoja na Chuo cha Maendeleo ya Jamii cha Tengeru pamoja na kuanzisha huduma rafiki kwa vijana, huduma zinazotolewa bure kwenye zahanati na vituo vya afya.

 Kwa upande wake Mratibu wa Afya ya Uzazi na Mtoto Mkoa wa Arusha, Belinda Mumbuli, amessma katika kipindi cha mwaka jana jumla ya wajawazito 94,582 walihudhuria kliniki na kati yao 12,540 ambao ni sawa na asilimia 13 walikuwa chini ya miaka 20.

Amesema katika kipindi hicho wananchi 281,887 walijitokeza kupata huduma ya uzazi wa mpango na kati yao vijana walikuwa 61,160 na kuwa wanaendelea kufanya makongamano kwenye jamii na shule kuhusu afya ya uzazi.

“Ukiangalia kundi la vijana kuanzia miaka 10 hadi 14 wameshaanza ngono hivyo bado tuna jukumu la kuelimisha jamii ukiangalia takwimu za mwaka jana kati ya mimba zilizoharibika miaka 10-14 ziliharibika tatu, miaka 15-19 ziliharibika 176 na mimba 612 zingine ni za vijana wenye umri kati ya miaka 20-24, tunahitaji elimu zaidi ili kusaidia vijana katika suala zima la afya ya uzazi,” amesema.

Naye, Kaimu Mratibu Uzazi wa Mpango Jiji la Arusha, Claudia Kinunda, anataja baadhi ya changamoto ni pamoja na imani potofu ya matumizi ya uzazi wa mpango,uelewa mdogo wa jamii kuhusu huduma rafuki kwa vijana,mimba za utotoni pamoja na wajawazito kuchelewa kuanza kliniki.

Mratibu wa huduma ya afya ya vijana na watoto halmashauri ya Arusha, Butolwa Bujiku, anasema katika kuhakikisha elimu hiyo inawafikia vijana wanashirikiana na viongozi wa ngazi ya jamii na kuhamasisha wazazi/walezi ili vijana watumie vituo kupata huduma za afya ya uzazi.

Anasema katika halmashauri baadhi ya changamoto ni pamoja na idadi ndogo ya wanaotumia njia za kisasa za uzazi wa mpango chini ya asilimia 30 katika maeneo ya Kiserian,Mwandeti na Engorora.

“Nyingine ni ushiriki mdogo katika kliniki ya huduma ya afya ya uzazi na mtoto chini ya asilimia 10 hasa maeneo ya Engorora,Imbibia,Kimnyaki,Kiserian na Lengijave,”anasema Buiku.

Awali, Mratibu wa afya ya akili mkoa wa Arusha, Charles Migunga,amesema kundi la vijana limekuwa likikumbana na changamoto mbalimbali zinazowasababisha wengine kujiingiza katika matumizi ya dawa za kulevya.

Aidha anawataka wazazi na walezi wenye vijana waliojiingiza katika matumizi ya dawa za kulevya kuwapeleka katika vituo vya afya ili wapatiwe matibabu.

“Vijana wanakutana na changamoto mbalimbali za kimaisha hivyo wengine kujikuta wanashindwa kuzitatua na kujiingiza kwenye matumizi ya dawa za kulevya,ndiyo maana leo tumekutana na ninyi waandishi wa habari ili tusaidiane kuelimisga jamii na kusaidia vijana hawa,”amesema Migunga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles