Na Malima Lubasha, Serengeti
Waumini wa Dini ya Kiislamu Wilaya ya Serengeti, mkoani wa Mara, wametakiwa kuendelea kutenda mema hata baada ya Sikukuu ya Eid El Fitr kwa kuwa mfungo wa mwezi wa Ramadhan ni kumcha Mungu na kuacha matendo mabaya.
Wito huo umetolewa na Sheikh wa Wilaya ya Serengeti, Juma Simba wakati akitoa hotuba ya swala ya Eid El Fitr iliyofanyika Aprili 10,2024 kwenye msikiti wa Masijid Noor Mugumu kuwa sikukuu hiyo ni ukamilifu wa mtu aliyefunga mwezi mtukufu wa Ramadhan hivyo matendo hayo mema yaendelee siyo kwenda kinyume chake.
Amesema waislamu kuendelea kutenda mema na wasitoke nje ya maadili ya uislamu.
Sheikh Simba amewataka waislamu kuwa na moyo wa subira na kuvumiliana badala ya kusengenyana kwa kumzungumza mtu ambaye hayupo.
“ Waislamu tunapokuwa watu wawili tuongee ya watu wawili badala ya kuzungumza ya mtu ambaye hayupo, ni tabia ambayo haipendezi kwa Mwenyezi Mungu, tupendane kwa mema kumcha Mungu kwani kufunga kunatufundisha kuwa na subira na mambo yote tunayofanya kwa wema”,amesema Sheikh Simba.
Ameongeza kuwa licha ya kunywa na kula vyakula halali kwa kufuata misingi ya dini ya kiislamu, kila muumini kusaidia wenye mahitaji kama vile yatima,wajane na wasiojiweza ili kupata baraka.
Naye Sheikh wa Kata ya Mugumu wilayani Serengeti, Mikidadi Idd, amesema sifa kuu ya muislamu ni kumcha Mungu na yule aliye na hofu ya kuogopa anaposikia habari za Mwenyezi Mungu ikiwamo kuacha starehe zinazokwenda kinyume na mafundisho ya dini.
Aidha baadhi ya waumini wa dini hiyo walioswali ibada ya Eid El Fitr wamesema kuwa funga yao wameitumia kwa kufanya toba na wanatarajia malipo mema kutoka kwa Mungu kulingana na yale waliyotenda katika mwezi mtukufu wa Ramadhan na mafundisho yote waliyoaswa na viongozi wa dini.