Na Ramadhan Libenanga, Morogoro
KATIBU wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda, ameachiwa huru baada ya kukaa mahabusu kwa kipindi cha zaidi ya miaka miwili.
Hata hivyo baada ya kuachiwa huru na Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Morogoro, Sheikh Ponda amesema licha ya kuachiwa ataendelea kupambana kupigania haki za Waislamu nchini.
Katika mazungumzo yake, Sheikh Ponda alisema amesikitishwa na kitendo cha Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), kuchelewesha haki yake ya kuwa huru.
Akizungumza jana baada ya kuachiwa huru na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa wa Morogoro, Marry Moyo, Sheikh Ponda alisema kukaa kwake ndani kwa miaka miwili na miezi mitatu kunamfanya kuona umuhimu wa mabadiliko ya Katiba iliyokuwa ikidaiwa na wananchi.
Alisema Katiba mpya inayohitajika ni ile ambayo ingeweza kupoka baadhi ya madaraka katika vyombo vya sheria na dola kama ilivyokuwa katika kesi yake ambapo dhamana yake ilizuiliwa na mtu mmoja tu bila sababu za msingi.
“Nimefurahi kupata haki yangu lakini bado nalalamikia haki yangu ya dhamana ilizuiliwa na Mkurugenzi wa Mashtaka bila sababu, huku wakijua kuwa sina kosa la kujibu.
“Kukaa kwangu ndani kwa kipindi cha miaka miwili na miezi mitatu kumenifanya kuona umuhimu wa mabadiliko ya Katiba iliyokuwa ikilalamikiwa na Watanzania. Hili tutaendelea kupambana nalo dhamana ni haki yangu lakini ilizuiliwa na mtu mmoja tu,” alisema Sheikh Ponda.
Awali Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Morogoro ilimwachia huru Sheikh Ponda, ambaye alikuwa akikabiliwa na tuhuma za uchochezi.
Akisoma hukumu hiyo jana, Hakimu Moyo alisema kuwa mahakama imejiridhisha baada ya kupitia vielelezo na mwenendo wa kesi iliyokuwa ikimkabili na kuona kuwa mtuhumiwa hana hatia, hivyo akaamuru aachiwe huru .
Mara baada ya maelezo hayo, Hakimu Moyo alisema kuwa kutokana na kifungu 235 kifungu kidogo cha (1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002 mahakama inaona mshtakiwa huyo hana kosa, hivyo inamwchia huru.
Hakimu Moyo alisema katika kesi hiyo, Jamhuri ilikuwa na mashahidi tisa pamoja na vielelezo saba, huku upande wa utetezi ukiwa na shahidi mmoja ambae alionekana kupingwa na upande wa Jamhuri kwa madai kuwa amekuwa akifuatilia mwenendo wa kesi.
Sheikh Ponda alikuwa akituhumiwa kutamka maneno ambayo yalionekana kuumiza dini nyingine (maneno ya kichochezi) na kufanya mkutano usio halali Agosti 8, 2013 maeneo ya Kiwanja cha Ndege mkoani hapa.
Mahakama hiyo iliweza kumfutia mshtakiwa shtaka namba moja la kukiuka masharti ya Mahakama ya Kisutu ya jijini Dar es Salaam kwa kuwa mtuhumiwa alikata rufaa na kuweza kushinda rufaa yake hiyo.
Baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi ya mkoani hapa kufuta shtaka namba moja, mshtakiwa alibakiwa na mastaka mawili ambayo alitakiwa kuyajibu na mara baada ya mahakama hiyo kupitia maelezo ya pande zote imeona mshtakiwa hana hatia.
Sheikh Katimba
Msemaji wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Rajab Katimba alisema Waislam nchini kote wamefurahia kutendeka kwa haki , japo haki hiyo ilicheleweshwa.
Alisema kuwa kesi ya Sheikh Ponda haikuwa na itikadi za kidini wala siasa ndio maana hata wanasheria wake walikuwa kutoka katika imani tofauti , hivyo amesema kuwa lengo lilikuwa kutafuta haki za kiimani.
“Wanachotaka Watanzania ni kuona keki ya nchi inaliwa na Watanzania wote bila kujali itikadi za kidini wala siasa,” alisema Katimba.
Sheikh Katimba awewataka wafuasi wa Ponda pamoja na waumini wa dini hiyo kuwa watulivu, kwa kuwa kiongozi wao ameshinda kesi yake ambapo walisema watakaa wote kwa pamoja ili kujua nini kiongozi wao anatakiwa kukifanya kwa sasa.
Wakili wake anena
Miongoni mwa mawakili watatu waliokuwa wakimtetea Sheikh Ponda ni Abubakar Salim, ambaye alisema anafurahishwa na maamuzi hayo, kwani mahakama imetenda haki japokuwa haki hiyo imecheleweshwa.
Alisema kama Serikali haitakubaliana na maamzi hayo na kuamua kukata rufaa wao wako tayari.
Salim alisema kwamba, watakaa na mteja wao ili kuona kama anahitaji kufungua kesi kuishtaki Serikali kwa kumpotezea muda, ikiwa ni pamoja na kumnyima dhamana waweze kuifungua ila kama atawasamehe hayo ni maamuzi yake mwenyewe.
“Tunashukuru mteja wetu ameshinda kesi ambayo naiona kama ilikuwa ya kutengenezwa na watu kwa manufaa yao. Waswahili walisema mwisho wa ubaya ni aibu sasa kama Ponda atafungua kesi ya madai sisi tupo tayari,”alisema.
Sheikh Ponda alizaliwa miaka 56 iliyopita alikamatwa Agosti 19, 2013 na kushtakiwa kwa makosa matatu na baadaye kufutiwa kosa namba moja na kubaki na mashtaka mawili.
Ponda alinyimwa dhamana kwa kile kilichodaiwa ni sababu za kiusalama kulingana na kosa lake. Ponda amekaa mahabusu kwa miaka miwili na miezi mitatu.