Na Brighiter Masaki, Dar es Salaam
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu, ameungana na wadau mbalimbali wa Michezo pamoja na tasnia ya habari katika ufunguzi wa msimu wa mashindano ya mpira wa miguu (Ndondo Cup).
Ikiwa ni msimu wa Mwaka 2021 ambapo droo iliambatana na maonyesho ya mavazi (Fashion Shoo), yalioonyesha jinsi wachezaji na mashabiki wanavyopaswa kuvaa wakiwa mchezoni.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Julai 2, 2021 katika ofisini za Clouds Mikocheni jijini Dar es Salaam, Shaka amesema wachezaji wajitaidi kukumbuka mchango wa wakongwe wa mpira.
“Tunacheza na kuangalia ligi mbalimbali, lakini tunatakiwa kutambua mchango wa wachezaji wakongwe waliocheza kipindi hicho amboa walituandalia mazuri tunayoyaona leo hii,”amesema Shaka.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Ndondo Cup, Shaffih Dauda amesema kuwa ligi za Ndondo Cup zitaanza Julai 4, mwaka huu katika viwanja vya Kines.
Ameongeza kuwa mechi za ufunguzi zitachezwa na vijana wa Mabibo pamoja na Manzese na baadae zitaendelea kama droo ilivyochezeshwa.
Ufunguzi huo umehudhuriwa pia na baadhi ya wabunge na viongozi wa vyama vya siasa, wadao wa mitindo pamoja na wasanii kutoka katika tasnia ya Bongo Fleva na Bongo Muvi.