29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

Sh bilioni 16.3 zatolewa kusaidia wanawake

 

Na RAMADHAN HASSAN-CHAMWINO


KATIBU Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. John Jingu, amesema kupitia Mfuko wa Kuwezesha Wanawake Kiuchumi, hadi sasa Serikali imetoa zaidi ya Sh bilioni 16.3.

Jingu aliyasema hayo alipokuwa akifungua maadhimisho ya Siku ya Wanawake Wanaoishi Vijijini iliyoadhimishwa kitaifa katika Kijiji cha Manchali B, Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma juzi.

Alisema katika maeneo ya vijijini, zipo changamoto nyingi hususani katika masuala ya afya, elimu, maji na huduma ya umeme.

“Zaidi ya asilimia 70 ya chakula kinachozalishwa nchini kinatoka katika maeneo ya vijijini na wazalishaji wakubwa wakiwa ni wanawake, hivyo kuboreshwa kwa miundombinu kutasaidia kuwakwamua kiuchumi,” alisema.

Akizungumzia juu ya maadhimisho ya siku hiyo, Dk. Jingu alisema lengo ni kubuni mikakati ya kutokomeza mila kandamizi kwa wanawake.

Alisema moja ya mila kandamizi ambayo imekuwa kikwazo kikubwa kwa maendeleo ya mwanamke ni pamoja na wazazi kuozesha watoto katika umri mdogo.

“Unakuta mtoto ana umri wa miaka 10 anaozeshwa na mzazi wake ili waweze kupata mali hali ambayo ni ukatili wa kijinsia kwani mtoto ana haki ya kupata elimu,” alisema.

Akisoma risala ya maadhimisho hayo, mmoja wa wanawake waishio vijijini, Joanitha Kaangwa, alisema wanakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo ukosefu wa huduma za afya pamoja na maji.

“Hapa kwetu tuna changamoto kubwa hasa katika huduma ya afya, hatuna zahanati na ujenzi unaendelea umefikia katika hatua za mwisho, lakini haujakamilika kwa zaidi ya miaka minane,” alisema.

Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Julias Mbilinyi, alisema siku hiyo imeadhimishwa kwa mara ya kwanza nchini tangu ianzishwe na Umoja wa Mataifa mwaka 2007.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles