Na UPENDO MOSHA
-ROMBO
SERIKALI imeziagiza halmashauri za wilaya nchini kusimamia fedha za mikopo ya vijana, wanawake na walemavu ambazo zinatoka na asilimia 10 ya mapato, jambo ambalo litasaidia kuthibiti upotevu wa fedha hizo na kuacha kuisababishia hasara serikali.
Agizo hilo lilitolewa jana na Ofisa Maendeleo ya Vijana kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi,Vijana,Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Amina Sanga wakati akizungumza kwenye kikao maalumu cha kuangalia utekelezaji wa agizo la Serikali la kutengwa kwa asilimia 10 ya mapato ya Halmashauri ya Wilaya ya Rombo, kwaajili ya maaendeleo ya vijana,wanawake na walemavu.
Alisema fedha hizo zimekuwa zikitolewa naSerikali kupitia halmashauri za wilaya, zimekuwa zikipotea na kuisababishia hasara kubwa Serikali kutokana na kutokuwa na usimamizi imara wa watumishi wa umma.
“Bado juhudi za makusudi zinahitajika katika usimamizi wa fedha hizo, ambazo zimekuwa zikitengwa na halmashauri kutoka katika mapato yake ya ndani.
“Katika fedha hizo asilimia nne ni kwa ajili ya vijana,asilimia nne kwa wanawake na asilimia mbili kwa walemavu…lakini nyingi zimekuwa zikipotea kutokana na uzembe wa usimamizi,”alisema.
Alisema pamoja na Serikali kutoa mwongozo wa fedha hizo kutengwa, bado baadhi ya halmashauri zimekuwa zikikiuka utaratibu huo.
“Tunaipongeza halmashauri ya wilaya ya Rombo kwa kutenga fedha hizi kwa uaminifu mkubwa kwani bado suala hili limekuwa ni gumu kueleweka kwa baadhi ya halmashauri zetu hapa nchini,”alisema.
Awali akizungumza katika kikao hicho, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Rombo, Magreth John alisema jumla ya Sh milioni 10 imetolewa kwa vijana mwaka 2016/2017 na Sh milioni 49.5 mwaka 2017/2018.
Alisema baada ya kutoa fedha hizo wamefanikiwa kupata marejesho ya zaidi ya Sh milioni 32 na kwamba jumla ya vijana 401 wamenufaika kutoka katika vikundi mbalimbali.
“Fedha hizi tumekuwa tukizikitenga kila mwaka baada ya makusanyo yetu ya ndani licha ya kuwepo kwa changamoto ya baadhi ya vijana kugawana fedha hizo na kufanya mambo mengine tofauti na tulivyokubaliana na kusababisha baadhi yao kupotea na fedha lakini bado tunawabana na wanarejesha vizuri.
“Pia tumefanikiwa kulipa deni letu la Sh milion 16 hivyo tunaomba fedha nyingine za mikopo zitolewe ili na sisi tuweze kuwanufaisha vijana kujikwamua kiuchumi,”alisema.