26.6 C
Dar es Salaam
Sunday, October 1, 2023

Contact us: [email protected]

Watoto 49 waliokuwa wakitumikishwa mashambani warejeshwa kwa familia zao

Na JANETH MUSHI

-KARATU

WATOTO 49 waishio wilayani hapa katika Mkoa wa Arusha,wenye umri kati ya miaka 10 hadi 17,waliokutwa wakitumikishwa katika mashamba ya vitunguu wakati wa masomo,wamerejeshwa kwenye familia zao huku wamiliki wa mashamba hayo wakipewa onyo kali.

Kauli hiyo ilitolewa juzi katika Kata ya Endabash na Ofisa Ustawi wa Jamii wa halmashauri hiyo, Abdallah Nyange wakati akizungumza katika maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika,yaliyoandaliwa na Shirika lisilo la Kiserikali la World Vision Tanzania.

Alisema katika kipindi cha mwaka 2018/19,kwa kushirikiana na wadau wengine wa maendeleo wilayani humo walifanya tathimini na kukuta watoto hao wakitumikishwa katika mashamba yaliyopo Tarafa ya Eyasi.

“Kuhusu watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi tumefanya operesheni tatu ili kuhakikisha wanapatiwa haki zao za msingi kwa kushirikiana na wadau katika kipindi cha mwaka 2018/19.

“Tumeondoa watoto 89 waliokuwa wakiishi mitaani na kuwaunganisha na familia zao huku wengine wakiunganishwa na elimu ya watu wazima na sasa hakuna watoto mitaani kabisa,”alisema.

Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi wa World Vision Tanzania-Endabash AP,Daniel Kirhima alisema kwa kutambua umuhimu wa kulinda watoto kupitia miradi mbalimbali wanayotekeleza wilayani humo,imeendelea kutoa mafunzo kwa wazazi,viongozi wa dini,walimu,vijana na watoto.

Alisema wametoa mafunzo ya haki za watoto kwa mabaraza 32 yenye idadi ya watoto zaidi ya 1000,kwenye Tarafa ya Endabash na Eyasi.

Pia alisema wameunda na kutoa mafunzo kwa kamati za ulinzi na usalama wa wanawake na watoto katika vijiji 32 vyenye zaidi ya wajumbe 500.

“World Vision inatambua juhudi za serikali pamoja na wadau wengine katika kuhakikisha watoto wanatunzwa,wanalindwa na kuendelezwa ili tuwe na taifa endelevu.

“Natoa rai kwa wazazi na walezi kutambua wao ndiyo wadau namba moja wa kujenga msingi wa watoto kwa kuhakikisha anampatia mtoto wake mahitaji muhimu,”alisema.

Awali, Mkuu wa Wilaya ya Karatu, Theresia Mahongo aliwaonya wazazi na walezi ambao wamekuwa wakiruhusu watoto kwenda kutumikishwa katika mashamba ya vitunguu na kwamba operesheni maalumu itaanza katika maeneo hayo.

“Tumemaliza tatizo la watoto wa mitaani,wazazi na walezi wapo kuna baadhi mnawatuma watoto kwenda kuwatafutia riziki na kufanya vibarua katika mashamba ya vitunguu, namwagiza Ofisa Tarafa wa Eyasi,pambana na wanaotumikisha watoto tusiwaonee haya,wakati huu wa likizo nasikia huko ndiyo mambo yamechachamaa,hatutaona aibu kuwashughulikia wazazi,”alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles