Na SAMWEL MWANGA – BARIADI
WAZAZI na walezi wametakiwa kuwahamasisha vijana wao kujiunga na vyuo vya Mafunzo ya Elimu ya Ufundi Stadi (VETA) kuchangamkia fursa za ujuzi katika fani mbalimbali.
Wito huo ulitolewa na Meneja Uhusiano wa VETA, Sitta Peter alipozungumza na wadau mbalimbali wa
maendeleo b mjini Bariadi.
Alisema vijana wengi nchini wamekuwa wakibaki nyuma na kushindwa kwenda vyuo vya ufundi kupata ujuzi ikizingatiwa shughuli nyingi za maendeleo kupitia miradi mbalimbali inahitaji watu wenye ujuzi.
Peter alisema fursa nyingi ambazo zinazotokana na ujuzi zimekuwa zikichangamkiwa na wageni kutoka nje ya nchi huku wenyeji wakibaki nyuma na kuendelea kulalamikia serikali juu ya ukosefu wa ajira.
‘’Asilimia 90 ya wanafunzi walioko katika vyuo vyetu si wazawa wa mikoa ya Shinyanga, Mara na Mwanza ispokuwa waliopo wanatoka mikoa ambayo haina vyuo, tunaomba jamii iwe na mwamko wa kuwapeleka watoto veta.
“Vijana walioko katika vyuo vyetu wahakikishe mafunzo wanayoyapata yanageuka kuwa mali kwa kuitumia kama fursa ya kuweza kujiajiri na kupambana na umasikini katika ngazi ya jamii na taifa kwa ujumla,” alisema.
Alisema hamasa ya kujiunga na mafunzo hayo ni ndogo huku fursa nyingi zimekuwa zikichukuliwa na watu kutoka mikoa mbalimbali ambayo haina vyuo vya ufundi.
Juma Ally ambaye ni mkazi wa Wilaya ya Maswa, alisema vyuo hivyo vikitumiwa vizuri vitasaidia kupunguza idadi ya vijana kuajiriwa kwa vile wanaweza kujiajiri wenyewe.