23.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali yatoa Pori la Vikindu kwa wananchi

maghembenewNa TUNU NASSOR – PWANI

SERIKALI imetoa eneo la Hifadhi ya Pori la Vikindu kwa wananchi, kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya huduma za jamii za Kijiji cha Kipala, Kata ya Mwandege mkoani Pwani.

Uamuzi huo umefikiwa baada ya kubainika eneo hilo ambalo awali lilikuwa likimilikiwa na Wizara ya Maliasili na Utalii, kuwa ni moja ya maeneo ambayo kwa vipindi tofauti yalitumiwa na wahalifu kama sehemu ya maficho yao kabla ya kudhibitiwa na Jeshi la Polisi siku chache zilizopita.

Akizungumza katika hafla fupi ya kuwakabidhi pori hilo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne  Maghembe alisema Serikali imeguswa na matatizo yanayowakabili wakazi wa eneo hilo zaidi ya 10,000 kukosa huduma muhimu za kijamii.

Alisema anashangaa jamii ya watu wanaohifadhi pori hilo kukosa zahanati, shule, soko na huduma nyingine za kijamii huku pori hilo likigeuka maficho ya wahalifu.

“Haiwezekani wanafunzi wanaoishi katika kijiji hiki kutembea kilomita saba kufuata shule Vikindu huku wajawazito na wagonjwa wakifuata huduma Mbagala,” alisema Profesa Maghembe.

Alisema baada ya kuona umuhimu wa huduma hizo ameamua kutoa eneo hilo litumike kujenga miundombinu ya huduma za kijamii.

“Nawakabidhi hili eneo lenye ekari 50 kwa ajili ya kujenga huduma hizo na kesho watakuja wataalamu kupima na kuainisha mipaka hivyo kuanzia sasa nalitoa kwenu.

“Nitamwomba Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi kutoa hati miliki ya eneo hilo kwa kijiji hiki na baada ya miezi mitatu tutatangaza katika gazeti la serikali kuwa pori la Vikindu ni mali ya wananchi wa eneo hilo,” alisema.

Awali akitoa taarifa Mbunge wa Mkuranga, Abdallah Ulega, alisema wanafunzi wanaoishi kijijini hapo hutembea kilomita saba kwenda shule iliyopo Kisenvule, jambo linalosababisha wengi kushindwa kumaliza masomo kwa utoro.

“Huduma nyingi za jamii katika eneo hili zinapata katika kata ya Mbagala mkoa wa Dar es Salaam hivyo tunahitaji eneo hili kwa ajili ya ujenzi wa zahanati, shule ya msingi na sekondari, kituo cha polisi, kituo cha mabasi na huduma nyingine za jamii,” alisema Ulega.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles