SERIKALI imetoa kauli kuhusu mwanafunzi wa Kitanzania aliyedhalilishwa mjini Bangalore nchini India, ikisema inafuatilia pamoja na taarifa zisizothibitishwa za kifo cha mwanafunzi mwingine Mtanzania aliyekumbwa katika vurugu hizo.
Mwanafunzi huyo wa kike mwenye umri wa miaka 21 ambaye jina lake halikutambuliwa mara moja, alikumbwa na kadhia hiyo baada ya mwanafunzi ambaye ni raia wa Sudan kusababisha ajali ya raia wa India.
Kauli ya Serikali iliyotolewa jana bungeni Dodoma ilikuja baada ya mwongozo ulioombwa na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo), aliyetaka kujua hatua ya Serikali baada ya tukio hilo.
“Naomba kwa ruhusa yako tutumie kanuni ya 47, lakini naomba tusiahirishe Bunge kwa kumtaka Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kanda na Kimataifa, aandae kauli ya Serikali na kuileta bungeni ya tukio lililotokea hivi karibuni India ambapo binti wa Kitanzania akiwa katika matembezi na wenzake alivamiwa katika mji wa Bangalore na kuvuliwa nguo na kutembezwa uchi barabarani,” alisema Zitto.
Alisema japo tukio hilo lilitokea Januari 31, mwaka huu, hadi jana Serikali ilikuwa haijatoa taarifa yoyote.
“Mpaka sasa Serikali haijatoa kauli yoyote ya tukio hilo lililotokea Januari 31 na limesambaa katika mitandao ya jamii jana na baadhi ya magazeti yametoa habari hiyo leo,” alisema Zitto na kuongeza:
“Kama tunavyofahamu kwamba sisi kama Watanzania ni lazima kulinda haki za Watanzania popote walipo, Waziri wa Mambo ya Nje alete taarifa ya Serikali ya jambo hilo kama limethibitishwa na kuitaka Serikali ya India kuomba radhi kwa yaliyompata Mtanzania huyu.”
Akijibu kuhusu mwongozo huo, Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kanda na Kimataifa, Balozi Dk. Augustine Mahiga, alisema taarifa hizo amezipata tangu juzi na zinafanyiwa kazi.
“Taarifa hizi tumezipata tangu jana (juzi) kwamba huko India mwanafunzi wa Sudan alimgonga na pikipiki mwanamke wa Kihindi, baada ya tukio hilo kulikuwa na fujo na vurumai iliyokuwa inawalenga wanafunzi wa Afrika wakiwemo wa Tanzania,” alisema Dk. Mahiga.
Alisema wanafunzi Watanzania waliodhalilishwa walikuwa wanne na mmoja wao aliyevuliwa nguo katika mitaa ya Bangalore ni msichana.
Akizungumzia hatua zilizochukuliwa na Serikali, Dk. Mahiga alisema Ubalozi wa Tanzania nchini India umepeleka dokezo kuonyesha ghadhabu za Tanzania kwa tukio hilo.
“Hatua ya pili kutaka Jeshi la Polisi la India kupeleka ulinzi mahususi katika maeneo yote ambayo wanafunzi wanaishi wakiwemo Watanzania.
“Kuchukua hatua za kipolisi ili uchunguzi madhubuti ufanyike kwa lile lililotokea la kuwadhalilisha wanafunzi na kuwapeleka hospitali, uchunguzi unafanyika,” alisema Dk. Mahiga.
Pamoja na hali hiyo, alisema kuna taarifa za kifo miongoni mwa Watanzania wanne waliolazwa hospitalini.
“Kati ya wale wanafunzi waliopelekwa hospitali, kuna taarifa ambazo si rasmi, lazima zithibitishwe, kwamba mmoja wa wale wanafunzi amefariki. Lakini bado tunataka kuthibitisha kama hilo limetokea, tunawasiliana na ubalozi wetu kule New Delhi na suala hili sisi kama Serikali tunalifuatilia kwa karibu sana,” alisema.
Baada ya Balozi Mahiga kutoa kauli hiyo, Mbunge wa Kasulu Vijijini, Augustine Holle (CCM), alisema kuwa alisoma katika mji wa Bangalore ambako alikumbana na visa hivyo na kuitaka Serikali itoe tamko la kulaani udhalilishaji huo.
Hata hivyo, Waziri Mahiga alisema ni mpaka Serikali ikamilishe taarifa ya matukio hayo, hasa taarifa ya mwanafunzi wa Tanzania kunyanyaswa na mwingine kufariki.
Wakati hayo yakiendelea nchini, taarifa kutoka nchini India zinaeleza kwamba watu watano wamekamatwa kwa tuhuma za kumshambulia na kumvua nguo mwanafunzi wa kike mwenye umri wa miaka 21 kutoka Tanzania.