HERIETH FAUSTINE NA IDDY ABDALLAH (RCT), DAR ES SALAAM
SERIKALI ya awamu ya tano imetakiwa kuwakamata na kuwashtaki wafanyabiashara wanaojihusisha na biashara ya meno ya tembo.
Imetakiwa ichukue hatua hiyo bila kujali utaifa, hadhi na mamlaka waliyonayo watu hao.
Mjumbe wa Kampeni ya Okoa Tembo wa Tanzania, Lameck Mkuburo, alisema kufanya hivyo kutasaidia kuvunja mtandao wa ujangili nchini.
Alikuwa akizungumza Dar es Salaam jana alipotoa wito kwa serikali jinsi ya kukabiliana na tatizo la ujangili.
Mkuruburo alisema miaka 50 iliyopita walikuwapo tembo wapatao 300,000 nchini na mwaka 2014 walikuwa 109,000.
Alisema hivi wamebaki 43,000 ambao ni asilimia 60 ya tembo waliokuwapo miaka mitano iliyopita.
“Tunaomboleza kwa upotevu wa maelfu ya tembo ambao walikuwa sehemu muhimu ya historia na alama ya taifa letu,”alisema Mkuburo.
Alisema tembo ni miongoni mwa vyanzo vikubwa vya pato la taifa katika sekta ya utalii ambako zaidi ya watu milioni moja hutembelea hifadhi za taifa kila mwaka.
Watu hao huchangia asilimia 17 ya uchumi wa pato la taifa, alisema.
Alisema juhudi zilizofanywa na serikali katika kukabiliana na tatizo la ujangili zinatambulika ikiwamo kuundwa mikakati ya taifa dhidi ya ujangili.
Hata hivyo, aliitaka Serikali kushughulikia chanzo kikubwa cha ujangili ambacho ni biashara ya meno ya tembo.
Alisema urafiki wa historia uliopo kati ya Tanzania na China unaweza kutumiwa kufunga masoko ya meno ya tembo katika nchi hiyo.