Na Jonas Mushi, Dar es Salam
SERIKALI imewataka wananchi kutoa maoni yatakayoiboresha sheria ya makosa ya mitandao ya mwaka 2015 iliyosainiwa hivi karibuni na Rais Jakaya Kikwete ili yasaidie kuiboresha.
Imesema licha ya sheria hiyo kusainiwa na Rais, bado kuna umuhimu wa kuiboresha katika baadhi ya vipengele vyenye upungufu.
Kauli hiyo imetolewa jana jijini Dar es Salaam na Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa, katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika ofisini.
Mkutano huo uliandaliwa maalumu kwa ajili ya kuufahamisha umma kuhusu kusainiwa kwa sheria hiyo na rais na kuelezea umuhimu wake, huku pia waziri huyo akiitumia fursa hiyo kukaribisha maoni ya wadau mbalimbali kwa ajili ya kuiboresha.
“Tunaomba wananchi tuipokee sheria hii kwa sababu ni nzuri na itasaidia sana kuwalinda, lakini pia kama kuna kifungu chochote ambacho kitaonekana kuwa na upungufu leteni ushauri au maoni wizarani, tutayatafakari na tutayafanyia kazi,” alisema Mbarawa.
Waziri Mbarawa alisema Tanzania si nchi ya kwanza kupitisha sheria ya aina hiyo kwa sababu ya uwepo wa maendeleo ya teknolojia ya mawasiliano kulikosababisha kuongezeka kwa uhalifu wa mitandao.
“Sisi siyo wa kwanza, Nchi za Uingereza, India, Malaysia, Uganda, Korea Kusini, Singapore, Mauritius, Afrika Kusini, Marekani na nyinginezo tayari zina sheria ya aina hii na inasaidia kuwapa wananchi haki wanapofanyiwa uhalifu wa mitandaoni,” alisema Profesa Mbarawa.
Sheria ya Makosa ya Mitandao ni moja ya sheria zilizokosolewa kwa kiwango kikubwa na wadau wa habari pamoja na makundi mbalimbali ya kijamii, kwa madai kuwa inalenga kubana uhuru wa vyombo vya habari pamoja na kubinya uwanja mpana wa ukusanyaji na utoaji habari kwa waandishi wa habari.