29.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali yashtukia utitiri wa asasi za kidini

Dr-Harrison-MwakyembeNA NORA DAMIAN, DAR ES SALAAM

SERIKALI imesema asasi za kidini zinaongezeka nchini kwa kasi isiyo ya kawaida, hali inayosababisha kuwapo wageni wengi wanaoweza kuhatarisha usalama wa Taifa.

Akizungumza na watendaji wa taasisi zinazohusika na usajili wa mashirika ya hiyari, kijamii na kidini Dar es Salaam jana, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe, alisema sehemu kubwa ya asasi hizo ni tegemezi kwa asilimia 100 kutoka kwa wafadhili wa nje.

Alisema kuna tatizo la kimfumo, kwani taasisi tatu za Serikali zimekuwa zikifanya kazi ya usajili bila kujali kinachofanywa na chombo kingine na kusababisha kuwapo utitiri wa asasi hizo.

“Hali si nzuri, usajili hauendani na kasi na tija ya Serikali hii, madhara yameanza kuonekana, ikibidi tutasitisha kwa muda usajili ili tufanye ukaguzi na kupata takwimu sahihi,” alisema Dk. Mwakyembe.

Alisema ziko asasi zenye anwani na zisizo nazo, na nyingine ofisi zimekuwa kwenye mikoba ya wachungaji na masheikh.

“Nyingine zikishasajiliwa zinapotea na kuibuka kwenye matamasha au katika uchaguzi mkuu, zinajivika majoho mawili na kuparamia majukwaa ya kisiasa,” alisema.

Alisema Serikali inaheshimu uhuru wa kuabudu ndiyo maana imekuwa ikizipa nafuu asasi hizo, hasa katika misamaha ya kodi, lakini baadhi ya watu wametumia mwanya huo na kufaidika na jasho la walipakodi wa Tanzania.

Aliagiza kila taasisi kutaja idadi kamili ya asasi ilizosajili, masharti ya kusajiliwa, sehemu kunakofanyika usajili, zieleze kama zina utaratibu wa kufuatilia mwenendo wa asasi husika na suluhisho la kudumu la tatizo la kughushi vyeti vya usajili.

Pia aliziagiza taasisi hizo kueleza mara ya mwisho walipofanya ukaguzi wa asasi husika, ofisi na vitendea kazi vya asasi hizo, kutaja ada za usajili, mfumo wa usajili ilionao na mapungufu ya kisheria kama yapo.

“Kama wewe ni msajili wa asasi za kidini, lazima ueleze ni mara ngapi Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imewahi kuomba uthibitisho wa usajili wa vyombo hivyo pale vinapoomba misamaha mbalimbali,” alisema.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Profesa Sifuni Mchome, alisema kama taasisi hizo zitabaini kuwapo na haja ya kufanyiwa marekebisho kwa baadhi ya sheria, ziwasilishe mapendekezo yao, lakini kwa hoja zinazoonekana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles