Na MWANDISHI WETU
DAR ES SALAAM
SERIKALI imeonya watu wanaojihusisha na vitendo vya udanganyifu katika sekta ya Bima ya Afya nchini ikisema watakaobainika watakuwa wametenda kosa la jinai.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Faustine Ndugulile alikuwa akizungumza katika mkutano ulioandaliwa na Umoja wa Kampuni za Bima ya Afya Tanzania (ATI) Dar es Salaam jana.
Alisema Serikali inatambua udanganyifu huo hufanywa na baadhi ya watoa huduma za afya na watu wanaotibiwa kwa mfumo huo.
Wakati mwingine vitendo hivyo hufanywa kwa ushirikiano kati ya wafanyakazi wasio waaminifu pamoja na wateja, alisema.
Dk. Ndugulile alionya kuwa wanaojihusisha na udanganyifu huo kwenye huduma za Bima ya Afya wanatenda kosa la jinai na adhabu yake ni kifungo na faini.
“Serikali ya awamu ya tano inapinga kwa vitendo rushwa na udanganyifu na yeyote anayejihusisha na vitendo hivyo huchukuliwa hatua kali za sheria. Serikali hii imeelekeza nguvu zake katika kujenga mfumo na taifa lenye uadilifu,” aliongeza.
Naibu waziri alitoa wito kwa kila mwananchi kuwa mlinzi wa sekta ya afya kwa kutoa taarifa sahihi za vitendo vya udanganyifu kwa vyombo husika wahusika wachukuliwe hatua kali za sheria.
Alisisitiza kuwa Serikali inathamini mchango wa kampuni za bima ya afya nchini na inaendelea kuhakikisha kuna mazingira rafiki ya ushirikiano kati ya sekta binafsi na sekta ya umma.
Awali, Mwenyekiti wa ATI, Suleiman Khamis aliipongeza Serikali kwa juhudi za kuboresha huduma za afya nchini ikiwa ni pamoja na kuhakikisha Watanzania wengi zaidi wananufaika na huduma bora ya bima afya.
Alisema majadiliano katika mkutano huo uliowahusisha wadau wa sekta binafsi na umma umehuisha utatuzi wa changamoto ya udanganyifu utakaoweka mfumo bora wa utoaji taarifa pamoja na kuwa na viwango sawia vya gharama ya huduma kwa bima afya.
Naye Elia Kajiba, aliyemuwakilisha Kamishna wa Shughuli za Bima (TIRA), Dk Baghayo Saqware aliwataka wadau wa sekta ya bima nchini kuhakikisha wanazingatia Sheria ya Bima ya Mwaka 2009.