24.5 C
Dar es Salaam
Thursday, May 23, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali yashinda rufaa kesi ya Komu EALA

Mbunge wa Moshi Vijijini (Chadema), Anthony Komu
Mbunge wa Moshi Vijijini (Chadema), Anthony Komu

Na ELIYA MBONEA-ARUSHA

JOPO la majaji watano wa Mahakama ya Rufaa ya Afrika Mashariki (EACJ), limekubaliana na hoja za Serikali katika rufaa ya kupinga ushindi wa Mbunge wa Moshi Vijijini (Chadema), Anthony Komu.

Kupitia kwa Wakili Mwandamizi Mark Mulwambo na Pauline Mdendemi, Serikali ilikata rufaa ikidai mahakama iliyompa ushindi Komu haikuwa na uwezo wa kisheria wa kutoa uamuzi kuhusu Bunge la Tanzania ambalo ni mwanachama wa EAC.

Katika kesi hiyo namba 7 ya mwaka 2012 iliyosikilizwa na kutolewa uamuzi na majaji watatu wa Mahakama ya EACJ, Komu aliiomba mahakama hiyo itoe tafsiri ya kisheria juu ya Bunge kukiuka Ibara ya 50 ya mkataba wa EAC katika uchaguzi wa wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), Aprili 17, mwaka 2012.

Rufaa hiyo ilisikilizwa na kutolea hukumu juzi na jopo la majaji watano wakiongozwa na Rais wa Mahakama hiyo, Jaji Dk. Emmanuel Ugirashebuja, Makamu wake Libore Nkurunzinza, Edward Rutakangwa, Aaron Ringera na Geoffrey Kyiryabwirwe.

Akisoma hukumu hiyo mjini hapa jana, pamoja na mambo mengine, Jaji Dk. Ugirashebuja alikubaliana na hoja za Serikali kuwa mjibu rufaa hakuwa na sifa za kuwasilisha maombi ya kuomba tafsiri katika mahakama ya chini.

Alisema badala yake maombi hayo yalipaswa kuwasilishwa na taasisi ya Serikali kama Bunge au Mahakama Kuu kama ambavyo marekebisho yalivyofanywa baada ya kesi ya Professa Anyang’ Nyong’ wa nchini Kenya.

“Haikuwa sahihi kwa mahakama ya chini kupokea na kusikiliza shauri hili. Hivyo tunakubaliana na hoja za Serikali kwa kutengua uamuzi uliotolewa awali.

“Kwa vile shauri hili ni muhimu si kwa Tanzania tu bali kwa nchi zote wanachama, mahakama hii inaziagiza pande zote mbili kubeba gharama zake za kesi,” alisema Jaji Dk. Ugirashebuja.

Akizungumza mara baada ya kusomwa kwa rufaa hiyo, Komu aliyekuwa mahakamani hapo, alisema kutokana na matokeo hayo amejipanga kumwandikia barua Spika wa Bunge, Job Ndugai ili aweze kuanza mchakato wa kubadili baadhi ya kanuni.

“Mimi ni mbunge, sina haja ya kufanya ligi dhidi ya Serikali au Bunge. Lakini ukiangalia mchakato wa hoja ambazo majaji wameziwasilisha, utaona faida kubwa ya shauri hili kusikilizwa hadi lilipofikia hapa.

Alisema kutokana na uamuzi huo, Serikali haipaswi kuendelea kusubiria hadi ikamatwe, badala yake inapaswa kufanya marekebisho ya kanuni ili haki iwe inatendeka.

Kwa upande wake, Wakili Edson Mbogoro aliyemwakilisha Komu, alisema hukumu ya rufaa hiyo haikuelekea kwenye stahiki za rufaa, badala yake ilishughulikia suala la kama mahakama ya chini ilikuwa sahihi kupokea na kushughulikia malalamiko ya mteja wake.

Alisema kutokana na kupitia hoja hizo, mahakama hiyo ilifikia hitimisho la kumuona Komu kama mtu binafsi ambaye anaelekezwa na Ibara ya 30 na 33 na 51 kuwa alipaswa kuendelea na kesi aliyoifungua Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma.

“Isipokuwa kama huko Mahakama Kuu wangefikia hatua ya kuomba tafsiri ya mkataba wa EAC, basi Mahakama Kuu ndiyo ingefanya marejeo kwenye Mahakama ya EACJ. Na suala hilo bado lingeamuliwa na Mahakama Kuu,” alisema Wakili Mbogoro.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles