Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, imekiri kupokea bajeti ya Sh milioni 80.1 kutoka kwa familia ya Aquilina Akwilini ambapo imesema baadhi ya matumizi hayatakubaliwa kwa kuwa hayagharamiwi na serikali.
Taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mwasu Sware, imesema kuwa bajeti waliyokabidhiwa na ambayo inasambaa katika mitandao ya kijamii ni makadirio yaliyoandaliwa na familia ya marehemu.
“Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia kwa Katibu Mkuu wake, Dk Leonard Akwilapo, imepokea makisio ya gharama za mazishi kiasi cha Sh 80,150,00 kutoka kwa msemaji wa familia hiyo, Festo Kavishe.
“Baada ya kupokea makisio hayo Dk. Akwilapo alitahadharisha kuwa kuna baadhi ya matumizi hayatakubaliwa kwa kuwa kisheria hayagharamiwi na serikali pia katika makisio hayo kuna gharama ambazo zilikuwa zimepewa makadirio ya juu.
“Kutokana na hali hiyo, Katibu Mkuu aliagiza kuwe na kikao kati ya wizara na ndugu wa marehemu ili kuweka sawa changamoto hizo na kuwa n abajeti ya pamoja ambapo kikao kilifanyika jana jioni na kufikia muafaka,” imesema taarifa hiyo.