Asifiwe George na Imani Nathaniel (RCT), Dar es Salaam
CHAMA cha Walimu Tanzania Mkoa wa Dar es Salaam, kimesema Serikali imeanza kulipa deni la madai ya walimu kiasi cha Sh 1,936,572,146.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa CWT wa mkoa huo, Amina Kisenge, alisema kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2013 hadi Julai 2015 walikuwa wanaidai Serikali kiasi cha Sh 3,916,432,471.
Alisema kwa sasa deni lililobaki ni Sh 1,979,860,325 ambazo bado walimu wanadai.
Alisema pamoja na changamoto hiyo nyingine ni mfuko wa PSPF kutowalipa walimu wastaafu kwa wakati na kudai kuwa walimu waliostaafu kuanzia Januari hadi Septemba 2015 hawajalipwa mafao yao.
“Kutokana na hali hiyo, tunatoa rai kwa Rais John Magufuli amalize usumbufu huu kwa watumishi waliotumikia Taifa kwa uadilifu ili waweze kulipwa mafao yao,” alisema.
Alisema kilio chao kikubwa kwa Rais Magufuli ni Serikali kupitia Mdhibiti wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) kuanzisha kanuni mpya (kikokotoo) cha 1/580 inayoonyesha mafao ya walimu yanayolipwa kwa mkupuo toka kanuni ya awali yaani 1/540.
Kisenge alisema jambo hilo halikubaliki, hata kama walimu walioko kazini sasa hawahusiki na kanuni hii kwasababu inaanza kutumika kwa wale walioajiriwa kuanzia Julai mosi mwaka 2014.
“Kwa sababu hii hatukubaliani na msimamo wa SSRA na tunayapinga mabadiliko haya kwa nguvu zote kwani watakaoathirika na kanuni hiyo ni walimu ambao ni watoto wetu.
“Eneo lingine ambalo ni kero kwetu ni walimu Mkoa wa Dar es Salaam kutopandishwa madaraja kwa wakati, pia wanaostahili kupandishwa madaraja kwa mwaka husika sio wote wanaopandishwa na wanaopandishwa hawarekebishiwi mishahara yao,” alisema Kisenge.
Aliitaja kero nyingine kuwa ni Wakurugenzi wa Manispaa kutotekeleza maagizo ya kupanua wigo wa madaraja ya walimu kama yalivyoainishwa kwenye waraka wenye kumbukumbu namba CAC 2015/22801/D ya Julai, 2014.