24.7 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali yakabidhi boti za kubeba wagonjwa Ukerewe na Geita, RC aonya

Na Clara Matimo, Mwanza

Katika kutatua changamoto ya wananchi wanaoishi visiwani maeneo ya wilaya za Ukerewe mkoani Mwanza na Geita kukosa huduma ya usafiri pale wanapougua na kutakiwa kufika hospitali zilizo nje ya wilaya hizo, Serikali imekabidhi boti mbili za kubeba wagonjwa na moja ya uokoaji kwa wilaya hizo.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel(katikati) akikata utepe kuashiria kupokea boti tatu za kusafirisha wagonjwa na uokoaji katika wilaya za Ukerewe na Geita Vijijini. kutoka kulia kwake ni   Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, Kanali Denis Mwila,wa pili kulia kwake ni Mbunge wa Jimbo la Geita Vijijini, Joseph Msukuma na wa kwanza kushoto ni  Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Songoro Marine  Transport Boatyard , Major Songoro. Picha  na Clara Matimo.

Boti hizo ambazo ni MV Ukerewe II –Kazi Iendelee na MV Nzera (Geita) ambazo kila moja imegharimu Sh Milioni 217.6 pamoja na boti moja ya uokoaji MV SAR IV ambayo imekarabitwa kwa Sh milioni 576 zimekabidhi leo jijini Mwanza kwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel .

Akipokea boti hizo kutoka kampuni ya Songoro Marine Transport Boatyard, Mhandisi Gabriel amesema wilaya ya Ukerewe yenye visiwa 38 ilikuwa inakabiliwa na changamoto ya kusafirisha wagonjwa kwenda hospitali za rufaa hivyo hatua hiyo ya serikali italeta nafuu kwa wananchi, huku akitoa onyo kwa  watakaozisimamia wazitunze na kuzitumia kwa lengo lililokusudiwa la kuokoa maisha ya wagonjwa. 

“Wala zisitumike kusafirisha bidhaa haramu ndani ya ziwa kwa kivuli cha kubeba wagonjwa, unaweza ukakutana na Ambulance inapiga king’ora barabarani  ukaipisha kumbe inapeleka magendo,  sasa haya sitaki kuyasikia kwenye hizi….niwaombe uongozi wa Ukerewe na Geita Vijijini mzitunze ili zidumu na ziendelee kutoa huduma stahiki iliyokusudiwa,” amesema Mhandisi Gabriel.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (Temesa), Mhadisi Japhet Maselle amebainisha kwamba boti hizo zimetengenezwa kwa viwango vinavyokubalika kimataifa  (IMO Standard) na zina uwezo wa kubeba Kilo 2,000 kila moja sawa na watu 12 kwa wakati mmoja, pia zina sehemu ya kumhudumia mgonjwa , vifaa maalum kwa ajili ya kumsaidia mgonjwa na mahali pa kukaa wauguzi na zimefanyiwa ukaguzi wa ubora na usalama na Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC).

Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, Kanali Denis Mwila, amesema wanategemea usafiri wa majini kufika jijini Mwanza zilipo hospitali za rufaa za Sekou Toure na Bugando, hivyo inapofika saa 10 jioni hakuna usafiri wowote wa umma kutoka huko, ambapo ujio wa boti ya kusafirisha wagonjwa utasaidia kuokoa maisha ya watoto, akina mama wengi na wananchi kwa ujumla wilayani humo.

Mbunge wa Jimbo la Geita Vijijini, Joseph Msukuma (CCM), amesema usafiri uliotolewa na Serikali ni mapinduzi makubwa kwa wananchi wake kwani itawasaidia kupata huduma kwa urahisi na haraka, ambapo ametoa wito kwa halmashauri ya wilaya ya Buchosa  kukarabati boti yao ambayo imekwama kutoa huduma kutokana na kuhitaji matenegenezo yatakayogharimu Sh milioni sita.

Kwa upande wake, Mwakilishi kutoka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi – Sekta ya ujenzi, Mhandisi Zilli Kihoko  amesema kukamilika kwa boti hizo kunazidi kutoa uhakika wa kuimarika kwa usalama na uwezo wa kukabiliana na changamoto za dharura kwani dhamira ya Serikali ni kutoa huduma bora za afya  kwa wananchi wake ili washiriki katika shughuli za uzalishaji mali na kukuza uchumi wa nchi.

Naye Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa mkoa wa Mwanza, Jamal Abdul, amesema  kukamilika kwa boti hizo ni utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya chama chake ya mwaka  2020-2025  chini ya uongozi wa  Mwenyekiti,  Samia Suluhu Hassan ibara ya 83  ambayo waliahidi kuendeleza na kuboresha sekta ya afya.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Songoro Marine  Transport Boatyard , Major Songoro  amesema  boti hizo zimejengwa kwa kuzingatia  ubora wa kimataifa huku akiishukuru Serikali  kwa kuendelea kuamini kampuni za wazawa na kuihakikishia kwamba  zikitunzwa vizuri  zina uwezo wa kudumu  zaidi ya miaka 25 hadi 30.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles