|Editha Karlo, Kigoma
Wananchi wa Kijiji cha Nyamidaho, wilayani Kasulu wameishukuru Serikali kwa kuwajengea kituo cha afya cha kisasa kitakachohudumia takribani watu 176,212 wa Tarafa ya Makere.
Akisoma risala yake mbele ya mgeni rasmi, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Brigedia Jenerali Mstaafu Emmanuel Maganga, Mkurugeni wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu Vijijini Mhandisi Godfrey Kasekenya amemtaka awafikishie salamu zao kwa Rais John Magufuli.
Amesema serikali kuu ilitoa Sh milioni 500 kwa ajili ya ukarabati wa kituo hicho ambapo wamefanikiwa kujenga jengo la wagonjwa wa nje (OPD) ambapo mchango wa nguvu za wananch ulikuwa Sh milioni 37.
“Jumla ya Sh mulioni 537 zimetumika katika ujenzi wa majengo sita ikiwamo wodi ya wajawazito na watoto wachanga, jengo la kuhifadhia maiti, maabara, jengo la upasuaji na wagonjwa wa nje,” amesema.
Akiweka jiwe la msingi katika kituo Brigedia Jenerali Maganga amewasifu wananchi kwa kushirikiana na Serikali katika kutekeleza ukarabati na ujenzi wa miundombinu ya kituo hicho ambapo pia amewakuwakumbusha na kuwahimiza wananchi kujiunga na Bima ya Afya ili waweze kufaidi uwepo wa kituo hicho karibu yao.
“Wananchi jiungeni na mfuko wa Bima ya Afya ili kuokoa gharama za matibabu, CHF iliyoboreshwa imeweka utaratibu mzuri wa matibabu ambapo sasa inaruhusu mfumo wa rufaa kutoka ngazi za chini za kutolea huduma hadi ngazi ya Mkoa tofauti na utaratibu wa zamani uliowezesha mgonjwa kupata huduma kwenye kituo kimoja kilicho karibu na mgonjwa,” amesema.