25.6 C
Dar es Salaam
Sunday, January 5, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Serikali yaja na mkakati wa kutokomeza Dengue

ANDREW MSECHU Na ELIZABETH HOMBO

-DAR ES SALAAM

SERIKALI kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, imetangaza mkakati wa kudhibiti ugonjwa wa homa ya dengue kwa kuangamiza mazalia yote ya mbu katika mikoa ya Dar es Salaam na Tanga.

Mikoa mingine iliyoathiriwa na homa hiyo ambayo pia itahusishwa kwenye mpango huo ni Morogoro na Pwani ambayo tayari imesharipotiwa kukumbwa na athari za ugonjwa huo.

Taarifa ya wizara hiyo iliyotolewa baada ya Waziri Ummy Mwalimu kutembelea eneo la Jangwani jana, ilieleza kuwa katika hatua za awali, hatua ya kuangamiza mazalia ya mbu wanaosababisha ugonjwa huo itafanyika kwa ushirikiano na wananchi kwa kunyunyizia dawa za kuua mbu wapevu kwa kutumia mashine kubwa.

Ilieleza kuwa Ummy amefanya maamuzi hayo baada ya mikoa hiyo kuathiriwa na ugonjwa wa homa ya dengue na kwamba Serikali inachukua hatua kukabiliana na homa hiyo.

“Nimeelezwa Mkoa wa Dar es Salaam unahitaji kununua lita 1,000 za dawa aina ya Acteric 500 na Icteric 300 kwa ajili ya kunyunyizia mbu wapevu katika mitaa.

“Ninawataka wakurugenzi wa manispaa kuhakikisha dawa hizi zinanunuliwa mara moja na kufanya upuliziaji katika maeneo yenye mbu,” alisema Ummy.

Pia aliwataka wamiliki na waendeshaji wa migahawa, baa, hoteli, saluni, gereji, shule, ofisi binafsi na za umma kukagua mazalia ya mbu katika sehemu zote zinazozunguka maeneo yao, kufukia madimbwi ya maji na kufanya usafi kwa ajili ya kuangamiza mazalia yote ya mbu.

Ummy alivitaka vituo vya kutoa huduma za afya vikiwemo vya watu binafsi kuzingatia taratibu na miongozo iliyopo ya kutoa taarifa kwa uongozi wa afya wa halmashauri kila siku wanapopima na kugundua kuwa mtu ana ugonjwa wa dengue.

Kwa upande wake, Naibu Waziri Dk. Faustine Ndugulile aliwataka watoa huduma za afya wasio waaminifu kutotoa majibu yasiyo sahihi ya dengue na kutoa dawa zisizostahili kwa ugonjwa huo.

“Tutaanza kuchukua hatua kali kwa watu wanaojirekodi na kusambaza picha za video zinazosema watu wanywe maji ya mipapai au kupaka mafuta ya nazi, tunasema ugonjwa huu hauna tiba, hivyo mtu yeyote anayeona ana dalili hizo suluhisho ni kufika kituo cha afya,” alisema Dk. Ndugulile.

Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abubakari Kunenge, ambaye aliambatana na mawaziri hao, alisema kama mkoa  watatekeleza maagizo yote na kuteketeza ugonjwa huo, hivyo kuhakikisha wanaanza kupuliza dawa kwenye maeneo ya mazalia na kutoa wito kwa wananchi kushirikiana kufanya usafi wa mazingira na kuondoa mazalia ya mbu kwa ustawi wa afya.

Kabla ya kutoa maagizo hayo,Waziri Ummy alilithibitishia gazeti hili kuwa hadi kufikia mwishoni mwa wiki wizara ilikuwa imeagiza lita 11,400 za viuadudu kwa ajli ya Mkoa wa Dar es Salaam.

“Mvua ikiacha tu kunyesha watapulizia ili kuangamiza viluwiluwi na mbu katika maeneo yote ambayo yana mazalia ya mbu,” alisema.

Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Maendeleo ya Taifa (NDC),  linalomiliki kiwanda cha viuadudu cha Tanzania Biolaviside Ltd, Profesa Damian Gabagambi, alisema ni kweli kwamba kwa Tanzania katika miaka iliyopita kulikuwa na tatizo kidogo kwa sababu hakuna aliyeona haja ya kununua dawa kutoka kiwandani hapo, lakini hivi karibuni tayari Wizara ya Afya iliagiza lita 200,000 za viuadudu kwa ajili ya matumizi ya ndani.

Profesa Gabagambi alisema baada ya kuagiza dawa hizo, kiwanda hakikuweza kuzitoa zote kwa pamoja kwa sababu kilikuwa na hifadhi ya lita 60,000 ambazo tayari zimeshachukuliwa zote, hivyo kinaendelea kuzalisha tani 140,000 ambazo bado wizara zinazidai.

Alisema hata katika halmashauri sasa, inaonekana nyingi zimeweka bajeti kwa ajili ya viuadudu vinavyotoka kiwandani hapo na tayari ugavi wa dawa hizo unaendelea.

UFANISI WA DAWA

Kuhusu ufanisi wa dawa hizo, Profesa Gabagambi alisema iwapo zitatumika ipasavyo kwa mujibu wa maelekezo, zina uwezo wa kumaliza kabisa mbu na kufanya maeneo na mazingira kuwa salama dhidi ya mbu.

“Iwapo zitatumika ipasavyo, dawa zetu zina uwezo wa kumaliza kabisa mbu kwenye mazalia, kumaliza mbu wanaoishi na hadi kwenye mayai yao, hivyo zinaweza kutokomeza kabisa kizazi cha mbu. Suala hili linahitaji usimamizi.

“Suala la msingi hapa, hili si suala la kumuachia mtu mmoja mmoja kwa sababu tatizo halitamalizika. Ni suala la nia na jamii nzima inatakiwa kushiriki. 

“Serikali inaweza kutoa agizo na kusimamia watu wote kushiriki kwa pamoja na hili likifanyika, mbu wote watakwisha na matatizo yanayotokea na mbu hao itakuwa historia,” alisema.

Alisema dawa za kiwanda hicho zimeonesha ufanisi wa kiwango cha juu na tayari nchi kadhaa zimekuwa zikiagiza dawa hizo za viuadudu kutoka nchini, hatua inayoleta matumaini kuhusu ubora wake.

Profesa Gabagambi alisema hivi karibuni Swaziland pia imekuwa miongoni mwa nchi zinazotumia dawa kutoka kiwandani hapo, baada ya kuagiza shehena ya dawa za Dola za Marekani milioni tano.

Alisema nchi nyingine ambazo zimekuwa zikinunua dawa za kiwanda hicho ni Burundi, Kenya, Rwanda, Msumbiji, Serbia, Sri Lanka, Angola na Niger.

NAIBU WAZIRI MANYANYA

Mapema wiki iliyopita, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhandisi Stella Manyanya alisema kuwa takribani lita 196,378  za kupambana na mbu zimeshauzwa katika nchi za  Angola na  Niger. 

Alisema pia nchi ya  Angola imeahidi mwezi ujao kununua lita nyingine  85,192.

“Kiwanda kinafanya kazi vizuri. Na kwa sasa tunaendesha kampeni ya kuwashawishi watu kutumia dawa za kuua mbu katika nchi jirani na zote zilizopo katika Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na  ambapo  jumla ya lita  466,278 zimeshauzwa ndani na nje ya nchi,” alisema. 

Kiwanda hicho kilijengwa na Kampuni ya Madawa na mahabara kutoka Cuba, LABIOFAM kufuatia ziara ya Rais wa Awamu ya Nne,  Jakaya Kikwete aliyoifanya nchini humo mwaka  2009, baada ya kuiagiza NDC kuusimamia mradi huo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles