23.3 C
Dar es Salaam
Sunday, June 16, 2024

Contact us: [email protected]

SERIKALI YAJA NA BAETI TRILIONI 32/-

Na WAANDISHI WETU – DAR ES SALAAM


 

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk. Phillip Mpango, amewasilisha mapendekezo ya mpango wa maendeleo wa taifa na ukomo wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2018/19, huku akiainisha maeneo ya vipaumbele.

Dk. Mpango aliwasilisha mpango huo mjini Dodoma jana mbele ya wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika maelezo yake, Dk. Mpango alieleza vipaumbele katika mwaka huo wa fedha, kwamba ni pamoja na     miradi ya kielelezo itakayopewa msukumo wa kipekee.

“Miradi hiyo itakayotekelezwa ni pamoja na kituo cha kuzalisha umeme wa maji katika Mto Rufiji, ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha standard gauge, kuboresha Shirika la Ndege Tanzania na ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Tanga.

“Miradi mingine ni uzalishaji wa makaa ya mawe na umeme wa Mchuchuma na chuma cha Liganga, uendelezaji wa shamba la miwa na ujenzi wa Kiwanda cha Sukari Mkulazi, ujenzi wa Kituo cha Biashara na Huduma Kurasini.

“Uendelezaji wa kanda maalumu za kiuchumi hususani, Bagamoyo na Kigamboni, uanzishwaji wa kiwanda cha kusindika gesi asilia kuwa kimiminika mkoani Lindi, kuongeza idadi ya wataalamu katika fani mbalimbali na kuimarisha shughuli za Shirika la Viwanda Vidogo (SIDO).

“Mingine ni kiwanda cha ngozi na bidhaa za ngozi, Karanga, mradi wa magadi soda ulioko Bonde la Engaruka, Kituo cha Zana za Kilimo na Ufundi Vijijini (CARMATEC) na viwanda vya Nyumbu na Mzinga.

“Miradi ya kufungamanisha maendeleo ya viwanda na maendeleo ya watu pamoja kuimarisha sekta ya elimu, afya, barabara, reli, barabara, viwanja vya ndege na usafiri wa majini,” alisema Dk. Mpango.

Akizungumzia sekta ya kilimo, Dk. Mpango alisema

Serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya umwagiliaji, itaongeza upatikanaji wa zana na pembejeo za kilimo, itaongeza huduma za ugani, itaboresha upatikanaji wa miundombinu ya hifadhi ya mazao na masoko.

“Pia itatatua vikwazo mbalimbali vinavyosababisha viwanda vya ndani vinavyotumia malighafi zitokanazo na kilimo kushindwa kushindana na bidhaa husika kutoka nje,” alisema.

DENI LA TAIFA

Kuhusu deni la taifa, Dk. Mpango alisema hadi kufikia Desemba mwaka jana, lilikuwa limefikia Sh trilioni 47.756 na kwamba tathimini zinaonyesha bado ni himilivu.

Kwa mujibu wa Dk. Mpango, deni la nje lilikuwa Sh trilioni 34.148, sawa na asilimia 71.5 na deni la ndani ni Sh trilioni 13.607, sawa na asilimia 28.5.

“Lakini, ongezeko la deni hilo kwa kipindi cha Juni 2016 hadi Desemba 2017 limetokana na mikopo mipya na mabadiliko ya kiwango cha ubadilishaji fedha.

“Uwiano wa deni la ndani na nje kwa pato la taifa kwa mwaka 2017/18 ni asilimia 34.4 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 56, hivyo deni bado lipo chini ya kiwango cha hatari,” alisema.

HALI YA UCHUMI

Kuhusu mwenendo wa uchumi, Dk. Mpango alisema umeendelea kukua katika viashiria vingi.

Katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Septemba 2017, uchumi ulikua kwa kiwango cha wastani wa asilimia 6.8.

“Kiwango hicho ni cha juu zaidi ikilinganishwa na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambazo ni Kenya (asilimia 6.1), Rwanda (asilimia 6.0), Uganda (asilimia 5.5), Burundi (asilimia 0.0) na Sudani Kusini (asilimia hasi 6.3).

“Kwa upande wa nchi zote za Bara la Afrika, kasi ya ukuaji wa uchumi, Tanzania ilikuwa ya tatu baada ya Ethiopia yenye asilimia 8.2 na Ivory Coast yenye asilimia 7.6.

“Ukuaji huo wa uchumi, umechangiwa na ongezeko la shughuli za uchimbaji madini na mawe, habari na mawasiliano, usafirishaji na hifadhi ya mizigo, uzalishaji viwandani na ujenzi.

“Kwa upande wa kilimo, katika kipindi cha Januari hadi Septemba 2017, sekta hiyo ilikua kwa asilimia 3.3 ikilinganishwa na asilimia 2.5 katika kipindi kama hicho mwaka 2016.

“Kutokana na hali hiyo, Serikali itaendelea kuimarisha miundombinu ya umwagiliaji, upatikanaji wa pembejeo za kilimo, huduma za ugani na maghala ya kuhifadhi mazao na upatikanaji wa masoko,” alisema.

Pamoja na hayo, alisema hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2017, mfumuko wa bei ulikuwa wastani wa asilimia 5.3 na umeendelea kupungua na kufikia asilimia 4.1, Februari mwaka huu.

Kuhusu akiba ya fedha za kigeni katika kipindi kinachoishia Desemba 2017, alisema imefikia Dola za Marekani milioni 5.9 ikilinganishwa na Dola za Marekani, milioni 4.3 katika kipindi kama hicho mwaka 2016.

Pamoja na hayo, Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT), imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kuongeza ukwasi katika uchumi na ukuaji wa mikopo yenye gharama nafuu kwa sekta binafsi.

“Kutokana na hali hiyo, mwenendo wa mikopo kwa sekta binafsi umeanza kuongezeka kutoka kiwango cha ukuaji hasi wa asilimia 1.5 Oktoba 2017 hadi ukuaji chanya wa asilimia 2.0 Januari 2018.

“Aidha mikopo chechefu imeanza kupungua kutoka asilimia 12.5 ya mikopo kwa sekta binafsi mwezi Septemba 2017 hadi kuwa asilimia 11.2 Desemba 2017,” alisema.

Kwa habari zaidi jipatie nakala ya gazeti la MTANZANIA.


- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles