27.1 C
Dar es Salaam
Saturday, June 22, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali yageukia zao la chai

Na Ramadhan Hassan, Dodoma

SERIKALI imeweka mikakati ya kuongeza uzalishaji wa zao la chai kwa kufufua mashamba yaliyotelekezwa na kujenga viwanda saba vya kuchakata zao hilo vitakavyomilikiwa na wakulima wadogo.

Hayo yameelezwa leo Jumanne Mei 21,2024 jijini hapa na Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde, wakati akizungumza katika Siku ya Chai Duniani.

Silinde amesema wanamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa kipaumbele katika kilimo.

Amesema Serikali imeweka mikakati ya kuendeleza zao la chai kwa kufufua mashamba yaliyotekelezwa katika maeneo mbalimbali.

Ameitaja mikakati mingine ni kuhakikisha inaweka miundombinu ya Umwagiliaji katika mashamba ya chai ili wakulima walime misimu yote.

“Tunamshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa kipaumbele katika sekta ya kilimo ikiwemo ongezeko la bajeti hadi kufikia sh. Trillion 1.2 Wizara ya kilimo tumekuwa mstari wa mbele kuhakikisha sekta hii ya chai inakuwa kwa kutoa ruzuku katika pembejeo za kilimo mbolea, kutoa miche na kuongeza uzalishaji wa mbegu,” amesema Silinde.

Aidha, Serikali imetoa mwezi mmoja kwa Wamiliki wa viwanda vya chai nchini kulipa madeni wanayodaiwa na wakulima wadogo wa zao hilo.

Amesema hadi kufikia Juni 20, mwaka huu wamiliki wote wa viwanda wanaodaiwa na wakulima wadogo wa zao la chai wahakikishe wanalipa madeni hayo ili Wakulima wanufaike na kazi waliyoifanya katika kipindi chote cha msimu.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Chai Tanzania, Rukia Mwango, amesema serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kuhakikisha zao la chai lina simama.

Alizitaja hatua hizo kuwa ni pamoja na kutoa fedha kwa ajili ya kujenga Viwanda Saba vitakavyomilikiwa na wakulima wadogo, kutoa fedha kwa ajili ya kufufua mashamba ya chai ambayo yametelekezwa kwa muda mrefu.

“Serikali ya Rais Dk. Samia haijalala inaendelea kufanya jitihada mbalimbali za kuhakikisha zao hili linasimama, ametoa fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Viwanda na sasa tupo katika hatua za manunuzi vitakavyomilikiwa na wakulima wadogo,” amesema Rukia.

Katika hatua nyingine alitaja changamoto zinazokabili zao la chai kuwa ni propaganda za baadhi ya watu ambazo zimechangia kudhoofisha soko la ndani la chai.

Amezitaja baadhi ya changamoto hizo ni kwamba chai inamadhara katika mwili wa mwanadamu.

Mwenyekiti wa Bodi ya Chai Tanzania, Mustapha Umande, amesema lengo la kuadhimisha siku ya chai duniani ili kutambua mchango wake katika kukuza ajira na kukuza uchumi wa mwananchi mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

Mwenyekiti huyo amesema serikali ya Awamu ya Sita imeweka kipaumbele kuhakikisha sekta hii inakuwa kutokana na umuhimu wake hasa kiafya ambapo husaidia kupungua athari za magonjwa ikiwemo kansa.

“Miaka mitatu ya hivi karibuni zao la chai limekumbwa na changamoto ikiwemo kushuka kwa bei na kupanda Kwa gharama za uzalishaji hivyo kuathiri mwenendo wake tunaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita haijatuacha tudondoke imeendelea kutoa ruzuku katika mbolea na kuhamasisha kilimo cha umwagiliaji,” amesema Mwenyekiti huyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles