28.2 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Serikali yafunguliwa kesi 13, madai ya bil 425 Mahakama za Kimataifa

Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA

WAZIRI wa Sheria na Katiba, Prof. Paramagamba Kabudi, amesema kwa kipindi cha miaka mitatu, mashauri yaliyofunguliwa nje ya nchi dhidi ya Serikani ni 13 ambapo madai yake ni Dola za Marekani 185,580,009.76 ambazo ni sawa na takribani shilingi bilioni 425 za Kitanzania.

Profesa Kabudi alisema hayo jana wakati akijibu swali la Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT Wazalendo), ambaye hata hivyo alipouliza swali la nyongeza, Kabudi alikataa kulijibu akisema ni mtego ambao uwe wa bahati mbaya ama kwa kutumwa, kamwe hatauingia.

Katika swali lake la msingi, Zitto alisema Tanzania inakabiliwa na mashauri mbalimbali kwenye mahakama za kimataifa kama vile ICSID, ICA London pamoja na ICC Paris.

“Kuanzia Novemba 2015, mashauri hayo ni mangapi kwa idadi, kwenye mahakama zipi na je, jumla ya madai ya mashauri hayo yote ni kiasi gani cha fedha kwa Dola za Marekani?

“Je, kuanzia mwaka 2000-2018 kumekuwa na mashauri mangapi dhidi ya Jamhuri ya Muungano, mangapi yameamuliwa, mangapi bado na mangapi Tanzania ilishinda.

“Je, kesi iliyofunguliwa na Kampuni ya Acacia Mining (LCIA Arbitration No. UN 173686 No. 87) huko London Uingereza ina madai gani na je, kwanini kuwe na kesi mahakamani wakati Serikali ilifanya mazungumzo na Barrick Gold ambao ni wamiliki wa Acacia?” alihoji Zitto.

Akijibu maswali hayo, Profesa Kabudi, alisema mashauri yaliyofunguliwa kuanzia Novemba 2015 ni 13 na yapo kwenye mahakama za usuluhishi za Permanent Court of Arbitration (PCA), London Court of International Arbitration (LCIA), International Center for Settlement of Investment Dispute (ICSID) na huko Johannesburg Afrika Kusini kupitia Sekretarieti ya UNICTRAL.

“Jumla ya madai katika mashauri hayo ni Dola za Marekani 185,580,009,76. Mashauri yote kwenye mahakama za kimataifa bado hayajatolewa uamuzi, hivyo takwimu halisi za madai na gharama ambazo Serikali inaweza kuwajibika kulipa itapatikana baada ya mashauri kuhusu kukamilika na uamuzi kutolewa.

“Kwa sasa hakuna kesi yoyote katika mahakama ya usuluhishi London iliyofunguliwa dhidi ya Serikali na Kampuni ya Acacia Mining Llc. Shauri Na. LCIA Arbitration UN 173686 lililotajwa na shauri UN 1736867 yamefunguliwa na kampuni za Pangea Minerals Limited na Bulyanhulu Gold Mining Limited, mtawaliwa.

“Utetezi wa Serikali kwenye kesi hizo umeshawasilishwa mahakamani. Makampuni hayo yameendelea na mashauri hayo kwa madai ya kulinda masilahi ya wanahisa hao,” alisema.

Akiuliza maswali ya nyongeza, Zitto alianza kutahadharisha kuwa swali lake la kesi zilizofunguliwa kati ya mwaka 2000 mpaka 2018 halijajibiwa.

Aliendelea kusema: “Kampuni za Pangea, Bulyanhulu, ni kampuni tanzu za Acacia, huwezi kuzitofautisha na Acacia, sasa kwanini tushtakiwe wakati tuna mazungumzo nao?

“Lakini pia vipi kuhusu kishika uchumba cha Dola za Marekani milioni 300 ambazo tulikuwa tumeahidiwa, pia sasa hivi Serikali imejifunza kuwa njia ilizotumia awali hazikuwa sahihi na sasa imejifunza?” alihoji.

Akijibu swali hilo, Profesa Kabudi, alisema masuala yote aliyoyasema Zitto yaliyo katika Mahakama za Kimataifa Serikali haitatamka chochote.

“Masuala yote yaliyosemwa na Zitto yapo chini ya mahakama kwa hiyo hayaruhusiwi kujadiliwa.

“Tamko lolote nitakalotamka hapa na likaingia kwenye Hansard (kumbukumbu za Bunge) litahadharisha hoja za Serikali na mtego huo uwe wa bahati mbaya ama wa kutumwa sintouingia kamwe. Ni mtego, uwe wa bahati mbaya ama kutumwa sintouingia kamwe,” alisema Prof. Kabudi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles