Na Mwandishi wetu,Njombe
Hatimaye Waziri wa TAMISEMI, Ummy Mwalimu amebariki maamuzi ya Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Njombe ya kutaka Makao Makuu halmashauri hiyo kujengwa katika kijiji cha Kidegembye kata ya Kidegembye na kuagiza zoezi la kuanza ujenzi lianze haraka iwezekanavyo.
Kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, Afisa Uhusiano wa halmashauri hiyo Lukelo Mshaura, amesoma taarifa ya mchakato wa ujenzi wa majengo ya utawala katika halmashauri hiyo ambapo amesema baadhi ya fedha zilizotolewa na serikali kwa ajili ya ujenzi wa makao makuu zilishanza kutumika hadi walipositishwa kuendelea.
“Baada ya baraza la madiwani kwa pamoja kukubaliana ujenzi ufanyike katika kijiji hiki cha Kidegembye baada ya serikali kuleta fedha tualianza kununua vifaa lakini tulivyoambiwa tusimame tuliviweka stoo kusibiri maelekezo mengine,”amesema Mshaura.
Tamko la kuunga mkono maamuzi ya madiwani hao amelitoa akiwa Mtwango wakati akizungumza na madiwani na watendaji mara baada ya kutembelea atika vijiji vya Kidegembye na Matembwe ambako imejengwa hospitali ya wilaya ambapo alisema hakuna sababu ya kuendelea kusubirisha jambo hilo ilihali serikali ilishatoa shilingi milioni takribani 900 kwa ajili ya ujenzi wa mkao makuu hayo.
Awali, mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Njombe Valentino Hongoli pamoja na Mbunge wa jimbo la Lupembe Edwin Swale wamemsisitizia waziri huyo kutokuwapo kwa mgogoro juu ya eneo la ujenzi wa makao makuu hayo huku wakisema wananchi wa Kidegembye wamejitolea kutoa eneo kubwa kwa ajili ya ujenzi huo.
Baadhi ya madiwani wa halmashauri hiyo akiwemo Roida Wandelage, Neema Mbanga na Paulo Kinyamagoha
wamepongeza maamuzi ya serikali kuridhia maamuzi yao huku wakitaka kuendelea kushughulikiwa kwa changamoto mbalimbali zikiwemo za miundombinu ya barabara pamoja na tatizo la wakulima wa chai kucheleweshewa malipo yao.
“Tunaishukiru serikali kwa kukubali kuanza ujenzi wa makao makuu ya halmashauri kwa sababu jambo hili lilitutesa tangu mwaka 2019,tulishindwa kuelewa kwanini maamuzi ya madiwani hayaheshimiwi,” amesema Roida Mwandelage.
Tangu mwaka 2019 serikali ilipotangaza kila halmashauri kuhamia katika maeneo yao ya kiutawala halmashauri ya wilaya ya Njombe ilikuwa ikitolea huduma katika kijiji cha Lunguya kwa muda hadi sasa serikali inapobariki maamuzi ya madiwani juu ya eneo la ujenzi wa makao makuu.