31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

CRDB Bank Marathon yakusanya Sh milioni 500 kusaidia afya, mazingira

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Shilingi milioni 500 zimekusanywa kupitia mbio za hisani za kimataifa zilizoandaliwa na Benki ya CRDB (CRDB Bank International Marathon) kwa mwaka 2021.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akimkabidhi mfano wa hundi ya Sh milioni 200 Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, Profesa Mohammed Janabi ambazo zimekusanywa kupitia CRDB Bank Marathon kusaidia upasuaji kwa watoto 100 wenye magonjwa ya moyo.

Fedha hizo zitapelekwa kwa watoto wenye uhitaji wa upasuaji wa moyo katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), kujenga kituo cha mawasiliano cha Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) na kusaidia utunzaji mazingira kupitia kampeni ya Pendezesha Tanzania.

Akizungumza wakati wa mbio hizo leo Agosti 15 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ambaye alikuwa mgeni rasmi ameipongeza benki ya CRDB kwa ubunifu huo na kuzitaka taasisi nyingine kuiga mfano huo.

“Serikali inasikia fahari kuona taasisi za kizalendo kama Benki ya CRDB zikiwa mstari wa mbele katika kusaidia kuboresha sekta za kijamii kama vile afya, elimu na mazingira. Mbizo hizi zinazofanyika kila mwaka ni fursa adhimu ya kuchangisha fedha kwa ajili ya kuwekeza katika ustawi wa jamii,” amesema Majaliwa.

Aidha amepongeza uamuzi wa Benki ya CRDB kuendelea kusaidia upasuaji wa watoto wenye magonjwa ya moyo kwani utapunguza makali ya gharama za upasuaji wa moyo ambazo watu wengi hawawezi kuzimudu licha ya Serikali kutoa ruzuku ya asilimia 80.

“Wazo hili la kuendelea kusaidia gharama za upasuaji kwa watoto ni uamuzi mzuri sana kwani hata asilimia 20 iliyobaki wazazi wengi hawana uwezo wa kuchangia. Hongereni kwa kurejesha tabasamu kwa watoto na kuwapatia tumaini la maisha,” amesema.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akimkabidhi mfano wa hundi ya Sh milioni 104 Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, Dk. Julius Mwaiselage, ambazo zimekusanywa kupitia CRDB Bank Marathon kusaidia ujenzi wa Kituo cha Mawasiliano.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, amesema mbizo za mwaka huu zimevuka lengo la ukusanyaji wa Sh milioni 500.

“Kati ya fedha zote zilizopatikana shilingi milioni 200 zimeelekezwa JKCI, Sh milioni 104 zimeenda ORCI na kiasi kilichobaki kimeelekezwa katika kampeni za utunzaji wa mazingira,” amesema Nsekela.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mawasiliano Benki ya CRDB, Tully Mwambapa, amesema mbio hizo zimeshirikisha zaidi ya washiriki 5,000 kutoka ndani na nje ambapo wakimbiaji wa kimataifa waliojisali kutoka nje ya Tanzania ni zaidi ya 700.

Amesema mbio hizo za CRDB Bank International Marathon zimeendelea kutambulika kimataifa baada ya kupatiwa ithibati na World Athletics na AMIS na kwa sasa zina hadhi sawa na mbio za Sanlam Cape Town Marathon za Afrika Kusini na Boston Marathon za Marekani.

Katika mbio hizo Paulo Ayanaye wa Kenya ameibuka kinara kwa kukimbia kilomita 42 kwa upande wa wanaume akitumia saa 2:15:28 wakati Mtanzania Shelmith Nyawira ameibuka mshindi kwa upande wa wanawake.

Aidha kwa mbio za kilomita 21 mshindi kwa upande wa wanaume ni Mkungo Panuel wa Kenya wakati kwa wanawake ni Pauline Esikon wa Kenya pia.

Katika mbio za kilomita 10 mshindi kwa upande wa wanaume ni Joseph Teophil wa Tanzania na kwa wanawake ni Transfora Musa wa Tanzania pia.

Aidha mbio za baiskeli kilomita 65 Masunga Duba wa Tanzania aliibuka mshindi kwa upande wa wanaume huku Swabra Abdallah naye wa Tanzania akiibuka mshindi kwa wanawake.

Washindi 32 katika mbio hizo wamejinyakulia jumla ya Sh milioni 50.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles