Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
SERIKALI ya Uingereza imempongeza Rais Dk. John Magufuli kwa jitihada zinazofanywa na Serikali yake katika ukusanyaji wa mapato na kukabiliana na vitendo vya rushwa.
Akizungumza jana baada ya kukutana na Rais Magufuli Ikulu Dar es Salaam jana, Balozi wa Uingereza nchini, Dianna Melrose, alisema juhudi za mapambano dhidi ya ufisadi, kubana matumizi na kudhibiti ubadhirifu wa mali za umma zinatekelezwa kwa vitendo na Serikali ya awamu ya tano ambapo ni mfano wa kuigwa.
Balozi Melrose alisema kutokana na hali hiyo, Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cmeroon, amevutiwa na utendaji kazi wa Rais Magufuli na kusisitiza kwamba nchi hiyo itaendelea kumpa ushirikiano wa karibu.
“Uingereza itaendeleza ushirikiano wa karibu uliopo kati yake na Tanzania katika nyanja mbalimbali za maendeleo,” alisema Balozi Melrose.
Kabla ya kukutana na balozi huyo wa Uingereza, Rais Magufuli alikutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Afrika Kusini hapa nchini, Thamsanqa Mseleku pamoja na Balozi wa Misri, Mohamed Yasser El Shawaf ambao waliihakikishia ushirikiano Serikali ya awamu ya tano.