Na Clara Matimo, Mwanza
Wadau wanaotetea haki za watoto wameonyesha kusikitishwa kwao na kuthiri kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia dhidi ya kundi hilo vinavyoendelea katika jamii na kuiomba Serikali kuweka mfumo sahihi wa kudhibiti matukio hayo.
Wadau hao ambao ni mashirika yasiyo ya serikali yanayojishughulisha kutete haki za wanawake na watoto la Kivulini na HAKIZETU ORGANIZATION wametoa ushauri huo Juni 16, mwaka huu jijini hapa wakati wa maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika yaliyofanyika kimkoa katika uwanja wa furahisha ambayo yaliongozwa na kauli mbiu isemayo ‘imarisha ulinzi wa mtoto, tokomeza ukatili dhidi yake, jiandae kuhesabiwa’.
Walisema ulinzi na usalama kwa mtoto bado ni changanoto kubwa kwani maeneo ambayo yanatarajiwa kuwa salama kwake kama nyumbani lakini ndiko anafanyiwa ukatili wa kubakwa ama kulawitiwa hata kuuwawa na ndugu wa damu kama baba au wa karibu ikiwemo wajomba na wafanyakazi wa nyumbani.
Mkurugenzi wa Shirika la Kivulini, Yasin Ally, alisema: “Takribani mwezi mmoja uliopita tumeshuhudia wimbi kubwa la vitendo vya ulawiti, ubakaji na mauaji ya watoto matukio mengi yakiwa yanafanywa na watu ambao tungetegemea wakiwa nao wako salamani lakini baadhi ya baba wanalawiti, wanabaka na kuuwa watoto wao, wajomba, wafanyakazi wa nyumbani.
“Hivi karibuni jijini Dar es Salaam yameripotiwa matukio mawili ambapo wasichana wa kazi za ndani wanatuhumiwa kuua watoto wawili, hivyo tunapoadhimisha siku hii tuangalie ni wapi tuweke mifumo ya ulinzi na usalama kwa mtoto kuanzia ngazi ya familia, mimi nadhani zoezi la ukusanyaji takwimu za sensa liende sambamba na kuainisha ni kiwango gani cha ukatili tulichonacho dhidi ya watoto serikali na wadau tukae pamoja tuangalie tunamlindaje mtoto, ulinzi nyumbani, maeneo ya shule, usafiri na ibada yakoje,” amesema.
Ally amefafanua kwamba wadau wamejitahidi kuwapa watoto elimu kuhusu stadi za kujitambua, kujilinda na kufichua ukatili wanapofanyiwa ingawa wengi wanaowafanyia vitendo hivyo wanawatisha wakisema endapo watatoa taarifa watawauwa lakini sheria nayo inachangamoto hivyo ameomba Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuifanyia marekebisho.
“Tunaona kuna kulegalega kwa sheria kuchukua mkondo wake sasa hivi wadau tumeiwezesha jamii kufichua na kuripoti polisi vitendo hivyo lakini ufanikishaji wa mashauri hayo mahakamani bado unasuasua au watu kujitokeza kutoa ushahidi ni changamoto,” amesema na kuongeza:
“Hata mifumo ya uendeshaji wa mashauri haya unamtaka mtoto aliyebakwa athibitishe pasipo kuacha shaka wakati kuna viungo vya mwili ambavyo hata mtu mzima hawezi kuvitaja waziwazi lakini mahakama inataka avitaje, akisema dudu mahakama inasema hakuthibitisha, kwa kweli tunaomba bunge lifanye marekebisho ya sheria kwenye kipengele hicho waipeleke hata kwenye muswada wa dharula ili tuendelee kuimarisha ulinzi wa watoto wetu,”amesema.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel, Mkuu wa Wilaya ya Magu mkoani humo, Salum Kalli, amesema serikali inaendelea kuimarisha jamii ili kupinga unyanyasaji na ukatili dhidi ya watoto kwa kupitia sera ya mtoto kutumia sheria zilizopo hivyo kufanya uelewa kwa jamii itambue namna ya kutumia hudumza za msaada wa kisheria kwa kutoa taarifa za ukatili kwa watoto hususani katika maeneo ya pembezoni.
“Licha ya idadi ya watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani kuendelea kuongezeka kama takwimu zinavyoonesha kuanzia mwaka 2018 hadi 2021 watoto walioingia mtaani walikuwa 806 kati yao wakiume wakiwa ni 703 wakike 103 bado serikali inafanya jitihada kwa kushirikiana na wadau kuwarudisha na kuwaunganishan na familia zao.
“Natoa wito kwa familia zote ambazo zimewatelekeza watoto wawatafute mahali popote walipo waungane nao wachukue jukumu la kuwalea katika maadili bora, wawape mahitaji muhimu, wawalinde waweze kuwa viongozi wa baadaye ili tuepuke kuwa na watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi, tukumbuke mtaa hauzai mtoto,” amesema Kalli.