24.6 C
Dar es Salaam
Saturday, September 7, 2024

Contact us: [email protected]

RC Mwanza awataka Wakurugenzi kutenga fedha za lishe kuepuka udumavu kwa watoto

Na Clara Matimo, Mwanza

MKUU wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel, amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri zote mkoani humo kutenga na kuwasilisha fedha za kutekeleza afua za lishe kwa wakati ili kuepuka udumavu kwa watoto na kutengeneza kizazi cha watu wenye ufahamu.

Mratibu wa Chanjo Mkoa wa Mwanza, Amos Kiteleja, akitoa taarifa ya utekelezaji wa chanjo za polia na UVIKO-19, mkoani humo katika kikao cha kujadili mambo mbalimbali ya afya.

Agizo hilo amelitoa Juni 13, mwaka huu wakati akifunga kikao cha kujadili mambo mbalimbali ya afya ikiwemo lishe, utekelezaji wa chanjo ya polio na Uviko-19 baada ya Afisa Lishe wa Mkoa huo, Sophia Lugumi, kutoa taarifa ya utekelezaji wa afua za lishe kuanzia Julai, 2021 hadi Machi, 2022 iliyobainisha kwamba miongoni mwa changamoto wanazokabiliana nazo ni pamoja na baadhi ya halmashauri kutotoa fedha zilizotengwa na serikali kwa watoto ili kutekeleza afua za lishe pia hazilingani na idadi ya watoto.

Mhandisi Gabriel amesema Serikali inatekeleza afua za lishe ili kutengeneza taifa bora la kesho kwa sababu watoto wanaokabiliwa na changamoto ya utapiamlo nao  wanategemewa kuendeleza nchi hapo baadaye ndiyo maana inawajali ili waweze kuimarika kiafya.

“Kuanzia leo sitaki tena kusikia kuna mkurugenzi yoyote ambaye hajapeleka fedha hizo tena kwa wakati, fedha hizo si za kujadili labda wakurugenzi hawajawaona watoto wanaokabiliwa na changamoto hiyo, afisa lishe hakikisha unawashirikisha wakurugenzi wote wa halmashauri ndani ya mkoa huu wafike hata kama ni wodini ili wawaone watoto hao naamini watawahurumia na watatambua umuhimu wa kutoa fedha hizo,” amesema Mhandisi Gabriel.

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dk. Thomas Rutachunzibwa, amesema tatizo la utapiamlo na ukosefu wa vitamini linasababisha watoto kuzaliwa wakiwa na vichwa vikubwa na mgongo wazi, linaathiri zaidi watoto wenye umri chini ya miaka mitano, akina mama wajawazito na wanaonyonyesha.

Akizungumzia utekelezaji wa chanjo za polia na UVIKO-19, Mratibu wa Chanjo Mkoa wa Mwanza, Amos Kiteleja, amesema kuanzia Mei 18 hadi 21, 2022 walikuwa na kampeni ya kuchanja chanjo ya kuzuia ugonjwa wa polio kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano ambapo walilenga kuchanja watoto 846,733 lakini walivuka lengo kwa kuwachanja watoto 926, 266.

“Chanjo ya Uviko 19 tulianza kuitoa  Agosti 3, mwaka jana hadi Juni, 11,  2022 tumeweza kuwachanja wananchi 479,000 angalau dozi ya kwanza haya ni mafanikio makubwa, tumeendelea kutoa na tutaendelea kuitoa hadi watanzania wote wachanjwe kwa sababu ugonjwa huo ni mbaya unaleta athari kubwa kiuchumi na kwa maisha ya Watanzania.

“Sasa hivi tumejiandaa kuchanja kwa kampeni kubwa ambayo tumelenga kuwachanja angalau watu 1,200,000 katika mkoa huu, tunatarajia kuianza Juni 16 hadi 22 mwaka huu tutafika maeneo mbalimbali ikiwemo nyumba kwa nyumba, sokoni, kwenye magulio, ofisi za taasisi za umma na binafsi  ni imani yetu tutaweza kuwafikia wananchi wengi na kuwachanja lengo letu ni kuweza kukata mizizi ya maambukizi,” amesema Kiteleja.

Nae Mkurugenzi Mkazi kutoka Shirika lisilo la serikali la Americares Tanzania linalojishughulisha kuisaidia serikali katika masuala mbalimbali ya afya, Dk. Nguke Mwakatundu, amesema elimu wanayowapa wananchi kuhusu umuhimu wa chanjo na  madhara ya ugonjwa wa UVIKO-19 imewezesha wananchi wengi kutambua thamani ya chanjo hiyo.

“Lengo letu ni kuisaidia serikali  ifanikiwe  kuutokomeza ugonjwa wa UVIKO-19 ndiyo maana ni wadau wa chanjo hiyo, tumekuwa tukitoa elimu kwa wananchi katika jamii na kuwaeleza chanjo zinazotolewa na serikali ziko salama na zinasaidia kuzuia kupata maambukizi ya ugonjwa huo tunavyoenda kwenye jamii na kutoa elimu tunaisaidia serikali kuwachanja wananchi wake huko huko kwenye jamii,  watu wengi  wanafikiwa badala ya kusubiri wapate chanjo hiyo kwenye vituo vya kutolea huduma za afya,” amesema Dk. Mwakatundu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles