Na FERDNANDA MBAMILA
-DAR ES SALAAM
SERIKALI imesema kwa sasa hali ya uchumi nchini iko sawa na umekuwa na kufikia asilimia saba, tangu Rais Dk. John Magufuli, alipoingia madarakani mwaka 2015.
Kauli hiyo ya Serikali imekuja siku moja baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kupitia Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe kusema kuwa hali ya uchumi kwa sasa ni tete tangu Rais Magufuli alipoingia madarakani.
Hata hivyo licha ya kuyumba kwa uchumi na kuongezeka kwa mfumuko wa bei duniani, Tanzania imeendelea kuongoza kwa ukuaji wa uchumi miongoni mwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo takwimu za Benki Kuu ya Tanzania (BOT) na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) zimetaja uchumi wa Tanzania kuwa imara.
Akizungumza jana na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Dk. Hassan Abbasi alisema Serikali imekuwa ikifanyakazi kwa kasi kwa ajili ya kuwaletea wananchi maendeleo.
Alisema ni vema Watanzania watambue kuwa hizi ni zama za kufanyakazi hivyo waache kulalamika na kingiza siasa.
“Tumeona tangu mheshimiwa Rais Dk. John Magufuli alipoingia tumesimama kwenye mstari ikiwemo kushudia maendeleo, sasa watu wafanyekazi kwani huu ni wakati wa kazi na si siasa,” alisema Dk. Abbasi.
Alisema takwimu za dunia kiuchumi zinaonesha tangu mwaka 2015 hadi Aprili 2016 uchumi wa Tanzania umekua kwa asilimia 3.1 ikilinganishwa na asilimia 3.5 kwa mwaka 2016.
Alisema uchumi wa Tanzania kwa miaka mitatu mfululizo sasa bado uko katika ukuaji usiopungua asilimia 7.0 hadi 7.2 ikiwa ni ukuaji wa juu katika ukanda wa Afrika Mashariki ambapo Rwanda inakua kwa asilimia 6, Uganda asilimia 5 na Kenya asilimia 6.4
Dk. Abbasi ambaye ndiye Msemaji wa Serikali alisema kuwa pamoja na hali hiyo pia uchumi umeendelea kukua, ambapo kwa Afrika Mashariki imekuwa ya kwanza na kwa Afrika Tanzania ni nchi ya nane kuchumi.
Alisema kwamba sambamba na ukuaji wa uchumi, Tanzania imeendelea kudhibiti mfumuko wa bei ambapo taarifa ya hivi karibuni zilizotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) zinaonesha kuwa mfumuko wa bei nchini umeshuka kutoka asilimia 6.1 Mei hadi kufikia asilimia 5.4 Juni mwaka huu.
“Sasa ni wakati wa kazi si siasa ambapo kwa sasa kwa upande wa miradi Tanzania imeanza kutumia gesi inayotokana na miradi ya umeme ya Kinyerezi I ambao unazalisha Megawati 150 tayari umekamilika na unafanya kazi na mradi wa Kinyerezi II hadi unakapokamilika utazalisha Megawati 180 ambapo bado haujaanza kutumika.
“Katika mradi wa ujenzi wa Barabara ya Juu (Fly over) ambao kwa sasa upo mbioni kukamilika na hivi karibuni utaanza kutumika, suala la elimu, Serikali hutoa kiasi cha Shilingi bilioni 18 kwa mwaka wa fedha ambapo katika kila mwezi fedha hizo hutumika katika shughuli za maendeleo na tayari unatumika,” alisema Abbasi.
Akizungumzia sekta ya habari Dk. Abbasi alisema kuwa tayari Tanzania imeridhia mikataba ya kisheria ukiwemo wa mwaka 1966 wa uhuru wa vyombo vya habari.
Alisema ingawa kuana mkataba mwingine wa marekebisho ya uhuru wa vyombo vya habari, uliotungwa mwaka 2016 ambapo umeanza rasmi kutumiaka mwaka huu.
Dk. Abbasi alisema alisema pamoja na baadhi ya Watanzania kulalamika hali ngumu ya uchumi lakini bado Tanzania inapiga hatua na inakadiriwa biashara 7, 277 zimesajiliwa kwa kipindi cha mwaka 2016/17 pamoja na kutoa kipaumbele kwa kusaidia vitendea kazi vya matibabu sambamba na kuboresha vituo vya afya.
“Vilevile alitoa wito kwa Watanzania waendelee kufanya kazi kwa bidii na kwa kujituma bila kujali itikadi zozote za kisiasa ili kuiwezesha nchi kukua kiuchumi katika ngazi ya juu zaidi.
“Hivyo kutokana na hatua ya serikali kuwa na hali nzuri ya uchumi, baadhi ya nchi zilizo endelea duniani zimeisifu Tanzania kwa ukuaji huo wa uchumi wa kasi,” alisema Abbasi
Juzi Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema tangu kuingia madarakani kwa Rais Dk. John Magufuli hali ya uchumi imekuwa tete, huku mauzo na manunuzi kwa bidhaa za nje ikiwemo mikopo ikiendelea kuporomoka.