29.9 C
Dar es Salaam
Monday, March 4, 2024

Contact us: [email protected]

MKOJO WA WEMA WAKUTWA NA VIMELEA VYA BANGI

NA KULWA MZEE-DAR ES SALAAM

MKEMIA, Elias Mulima, amedai mahakamani kuwa mkojo wa mrembo wa zamani wa Tanzania (2006), Wema Sepetu ulibainika kuwa anavuta bangi, baada ya kufanyiwa uchunguzi.

Mulima ambaye anatoka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, alidai hayo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam alipokuwa akitoa ushahidi upande wa Jamhuri katika kesi ya kukutwa na msokoto wa bangi inayomkabili Wema na wenzake wawili.

Shahidi huyo wa kwanza, akiongozwa na Wakili wa Serikali, Constantine Kakula alidai hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu,Thomas Simba.

Alidai Februari 8, mwaka huu, alipokea sampuli ya mkojo wa Wema na Februari 6, alipokea majani ambayo alifanyia uchunguzi kujua kama yalikuwa dawa za kuleya au laa.

“Wema aliletwa ofisini kwa Mkemia na Inspekta Willy na WP Mary, alipofika nilimfanyia usajili na kumpa namba ya maabara 321/2017.

“Walimleta kwa sababu walitaka Wema apimwe mkojo na nilimpa kontena maalumu na kumpatia WP Mary ambaye aliongozana naye hadi kwenye vyoo, akatoa sampuli ya mkojo.

“Baada ya kupatikana mkojo, nilipokea sampuli hiyo na kuendelea na uchunguzi ambapo hatua ya kwanza ni kuangalia chembechembe za dawa za kulevya  ndani ya mkojo wa Wema na baada ya uchunguzi nilibaini kuna dawa za kulevya aina ya bangi,”alidai.

Mulima alidai, kiutaalamu bangi inaweza kuonekana kwenye mkojo  ndani ya siku 28.

Alidai baada ya kuthibitisha anatumia bangi, aliandaa taarifa ya mchunguzi ambayo aliisaini yeye mwenyewe na ikathibitishwa na Kaimu Mkemia Mkuu wa Serikali, Februari 8, mwaka huu.

Shahidi huyo ambaye ni msimamizi wa maabara, anafanya uchunguzi wa kitaalamu wa sampuli za dawa za kulevya, milipuko na sampuli zinazodhaniwa kuwa na sumu, aliendelea kudai  February 6, akiwa ofisini kwake alipokea kielelezo kutoka Jeshi la Polisi Tanzania kupitia kwa  D/Koplo Robert kikitakiwa kufanyiwa mchunguzi kuthibitisha ni dawa za kulevya aina ya bangi ama la.

Alidai alikipokea kwa njia ya fomu DCEA 001, akakisajili na kukipa namba ya maabara 291/2017.

Alidai alifungua na kukuta msokoto mmoja na vipisi viwili ndani yake na  majani yadhaniwayo kuwa ni bangi.

“Niliyapima na kuyakuta yana uzito wa gramu 1.08, nilifanya uchunguzi kwa kutumia kemikali na kubaini ni bangi,”alidai.

Shahidi alipotakiwa kuzitambua taarifa alizoandika kama zake, alidai anaweza kuzitambua kwa sababu ina saini yake, mhuri wa moto na namba ya maabara na akaomba kuitoa mahakamani kama kielelezo cha ushahidi.

Wakili Peter Kibatala, anayemtete Wema, alipinga  ripoti hiyo isipokelewe  kwa sababu haijakidhi mahitaji ya kifungu cha 63 cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (CPA) sura ya 20  iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Kibatala, alidai  kifungu hicho kinaeleza utaratibu wa kufanya mchunguzi wa kitabibu kwa mshtakiwa ambaye yupo chini ya ulinzi, kuwa  lazima polisi awasilishe maombi mahakamani.

Kibatala, aliomba ripoti hiyo ikataliwe kwa sababu hakukuwa na ombi wala amri kutoka mahakamani.

Pia alipinga ripoti hiyo kupokelewa kwa sababu haijaambatanishwa na fomu namba DCEA 001.

Kutokana na hoja za Kibatala, Wakili Kakula alidai fomu  yenye namba 001 inatumiwa na  polisi wanapopeleka sampuli  na fomu namba 009 ni taarifa ya Mkemia na kwamba fomu moja, haitegemei nyingine kwa kuwa zinaandaliwa na watu tofauti.

Kakula, alidai  sheria haijasema muda wote ni lazima maombi yapelekwe mahakamani amri itoke ndiyo mshtakiwa afanyiwe mchunguzi wa kitabibu, ila pale ambapo mshtakiwa hataki polisi wanaweza kufanya maombi mahakamani.

Baada ya kusikiliza mabishano hayo ya kisheria, Hakimu Simba aliomba mahakama ipate nafasi ya kuzipitia nyaraka zinazobishaniwa, uamuzi utatolewa Agosti 4, mwaka huu.

Washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka mawili ya kukutwa na kiwango kidogo cha dawa za kulevya na kutumia dawa za kulevya.

Inadaiwa Februari 4,2017 katika makazi ya Wema huko Kunduchi Ununio,washtakiwa walikutwa na msokoto mmoja na vipisi vya bangi vyenye uzito wa gramu 1.08.

Kwa upande wa Wema, yeye anadaiwa Februari Mosi,mwaka huu katika  eneo lisilojulikana Dar es Salaam,  alitumia dawa za kulevya  aina ya bangi.

Washtakiwa katika kesi hiyo, ni Wema na wenzake wawili ambao ni Angelina Msigwa na Matrida Seleman Abbas.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles