26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali: Mradi wa Timiza Malengo unalenga kuwasaidia wasichana kutimiza ndoto zao

Na Nadhifa Omary, Tanga

SERIKALI imesema niwajibu wa kila msichana kutimiza ndoto zake hivyo ndio maana imekuja na mradi wa Timiza Malengo unaolenga kuwafikia wasichana balehe na wanawake vijana wanaotoka katika mazingira hatarishi.

Hayo yamebainishwa jijini Tanga Mei 29, 2022 na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu(Uratibu, Sera na Bunge), Ummy Nderiananga wakati wa ziara ya kutembelea utekelezaji wa mradi wa Timiza Malengo wenye lengo la kuwafikia wasichana balehe na wanawake vijana wanaotokea katika mazingira hatarishi ya kupata maambukizi mapya ya Virusi Vya UKIMWI.

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Uratibu, Sera na Bunge, Kaspar Mmuyaakizungumza na wanafunzi pamoja na wazazi wa shule ya msingi Majani mapana, kushoto kwake ni Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu(Uratibu, Sera na Bunge), Ummy Nderiananga akifuatiwa na Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Hamshim Mgandila na kulia kwake ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji TACAIDS, Jumanne Issango.

Akizungumza na wananchi wa Mkoa wa Tanga baada ya kutembelea shule ya Sekondari Nguvu mali na shule ya Msingi Majani Mapana,  Naibu Waziri Ummy amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu haitaki kuona mtoto wa kike akishindwa kutimiza malengo yake.

“Serikali ya awamu ya sita inayogozwa na mheshimiwa Samia Suluhu Hassani haitaki kuona mtoto wa kike anashindwa kufikia ndoto zake, ndiyo maana, Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Tume ya kudhibiti UKIMWI Tanzania(TACAIDS) wameona umuhimu wa kuratibu mradi huu kwa kushirikisha walimu ambao tayari wameisha elimishwa namna ya kuwafundisha vijana hao waliopo mashuleni.

“Lakini pia hata walimu ambao hawakuweza kushiriki mafunzo  haya hujengewa uelewa na walimu walioshiriki katika mafunzo lengo likiwa ni elimu hiyo kuwafikia vijana wote kwa urahisi, hivyo mnawajibu wa kuhakikisha kuwa mnasoma kwa bidii ili kuyafikia malengon yenu ambayo yatakuwa na faida kwenu na taifa kwa ujumla hapo baadae,” amesema Nderiananga.

⦁Kaimu MKurugenzi Mtendaji wa TACAIDS, Jumanne Issango akizungumza na wananchi walioshiriki katika kikao cha Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Uratibu, Sera na Bunge alipotembelea Mkoani Tanga Kufuatilia utekelezaji wa Mradi ya Timiza Malengo.

Amefafanua kuwa mradi huo unawalenga wasichana walio ndani na nje ya shule ambapo afua zinatekelezwa kulingana na makundi yao ikiwamo kupewa elimu ya afya ya uzazi na namna ya kujikinga na VVU.

“Vijana  walio shuleni wanapewa elimu ya afya ya uzazi na kujikinga na VVU shuleni na walio nje ya shule wanapewa afua zao ambazo zinawasaidia kubaki salama na kujiboresha kiuchumi kwa ajili ya kuzifikia ndoto zao,” amesema Nderiananga.

Mikopo kwa vijana

Mbali nakuzungumza na wanafunzi hao waliko shuleni, Naibu Waziri huyo pia alitembelea vikundi vya Watu wanaoishi na Virusi Vya UKIMWI (WAVIU) na kuona kazi mbalimbali wanazofanya kwa ajili ya kujiingizia kipato ambapo ameziagiza Halmashauri nchini kutenga fedha kwa ajili ya kuwawezesha WAVIU.

“Niwapongeze sana kwakuwa nimeona mnafanyakazi nzuri sana, na hapa nizielekeze halmashauri za Wilaya kote nchini kuona umuhimu wa kutenga sehemu ya fedha za mapambano dhidi ya UKIMWI kwa ajili ya kuviwezesha vikundi vya WAVIU kufanya shughuli zao za maendeleo vizuri,” amesema Nderiananga.

Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Uratibu, Sera na Bunge, Ummy Nderiananga akisisitiza jambo wakati anazungumza na watendaji wa Mkoa na Tanga (hawapo katika picha) wakati wa ziara yake ya Siku moja mkoani Tanga Mei 28, 2022 yenye lengo la kufuatilia Progaramu ya Timiza Malengo inayolenga kuwafikia wasichana balehe na wanawake vijana wanaotokea katika mazingira hatarishi ya kupata maambukizi mapya ya VVU.

Awali, akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mradi huo mkoani Tanga,  Meneja Mradi wa Timiza Malengo, Maricella Kawago alisema mradi huo umeibua waelimisha rika kutoka kata 27 za Jiji la Tanga na kuwapatia mafunzo maalum kwa ajili ya kuwafikia mabinti wenzao walio katika hatari ya kupata maambukizi ya VVU na UKIMWI sambamba na walio nje ya mfumo wa elimu kupitia program ya TASAF III na nje ya TASAF na kuwawezesha taulo za kike.

“Mradi wa Timiza Malengo unatekelezwa kwa miaka mitatu (2021-2023) katika mikoa mitano ya Dodoma, Geita, Morogoro, Singida na Tanga, katika mikoa hiyo mradi unatekelezwa katika Halmashauri 18 ambazoni Bahi, Chamwino, Kongwa na.

“Nyingine ni Mpwapwa, Kondoa Mji, Kondoa, Dodoma Jiji, Morogoro, Ifakara, Malinyi, Mlimba, Geita, Chato, Singida Manispaa, Singida , Ulanga, Tanga Jiji.

“Hivyo, kwa Tanga mradi huu unatekelezwa kwa kushirikiana na Shirika la Amref na Halmashauri ya Tanga Jiji kuwafikia Wasichana Balehe na Wanawake Vijana wenye umri wa miaka (10-24) waliopo ndani na nje ya shule,” amesema Kawogo.

Katika hatua nyingine, Kawogo amefafanua kuwa afua zilizozilizotekelezwa ni pamoja na zile za kitabibu, huduma rafiki za VVU na UKIMWI, uzazi wa mpango, uchunguzi wa magonjwa ya ngono, elimu na taarifa muhimu za afya na afua za mawasiliano ya mabidiliko ya tabia.

Amezitaja afua nyingine kuwa ni elimu ya afya ya uzazi, elimu ya matumizi sahihi na endelevu ya kondomu na ugawaji wa kondomu, elimu rika katika vikundi na elimu ya umuhimu wa kupima VVU.

“Pia kuna afua nyingine ambazo ni za kimiundombinu, uwezeshaji kiuchumi, ugawaji wa sodo (taulo za kike) mashuleni, msaada wa kuripoti na kudhibiti ukatili wa kijinsia,” amesema Kawogo.

Naye Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Uratibu, Sera na Bunge, Kaspar Mmuya amesema Baraza watu wanaoishi na VVU ambao wamejitokeza na kujitangaza na kusema wako tayari kushirikiana na serikali kutoa elimu (NACOPHA) ni muhimu.

“Baraza la watu wanaoishi na VVU ni muhimu kwakuwa wamekuwa msaada sana hata kushawishi na kurejesha WAVIU wengine walioacha kutumia dawa kwa sababu mbalimbali.

“Hivyo, ni muhimu miradi yote inayokuja na inahusu mwitikio wa UKIMWI, NACOPHA ishirikishwe kwakuwa kazi wanayoifanya ni kubwa sana,” amesema Mmuya.

Awali, Kaimu Katibu Tawala Msaidizi Afya Mkoa wa Tanga, Dk. Clemence Marcell alisema kuwa maambukizi ya VVU yamepungua kutoka asilimia 3.5 mwaka 2020 hadi kufikia asilimia 3.2. kwa mwaka 2021.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania, Jumanne Issango ameshukuru jitihada zinazotekelezwa na Mkoa wa Tanga katika kuhakikisha maambukizi yanapungua lakini kwa ushirikiano wanaouonesha katika afua zinazotekelezwa na programu ya Timiza Malengo.

“Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania ni Mratibu wa mwitikio wa UKIMWI nchini, ambapo wajibu wake pia ni kuhakikisha raslimali za kutekeleza afua za mwitikio wa UKIMWI zinapatikana, sisi tunaendelea kwa kushirikiana na wadau kutekeleza wajibu wetu lakini pia suala la UKIMWI sio la mtu mmoja, hivyo ushirikiano wetu utafanya tufikie mlengo ya kumaliza UKIMWI ifikapo 2030,” amesema Issango.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles