25.2 C
Dar es Salaam
Monday, April 22, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali lawamani

Jakaya Kikwete
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete

NA PATRICIA KIMELEMETA, DAR ES SALAAM

WANANCHI walio wengi wameonekana kuwa na imani ndogo na maofisa wa Serikali za Mitaa na Vijiji katika kushughulikia masuala yao.

Pia sekta ya maji na umeme ni miongoni mwa taasisi rasmi za serikali ambazo wananchi hawana imani nazo.

Kwamba wananchi wanaona taasisi hizo zinawarudisha nyuma kimaendeleo kwa sababu zimeshindwa kutatua kero zinazowakabili.

Kutokana na hali hiyo, hawaoni kama wanao uwezo wa kuishawishi Serikali, hivyo wengi wameamua kufuata njia zisizo rasmi za kufanikisha mambo yao wenyewe.

Hata hivyo, wananchi walio wengi bado wana imani na utendaji kazi wa Rais Jakaya Kikwete.

Hayo yamebainishwa na ripoti ya utafiti iliyotolewa jana na Taasisi isiyokuwa ya kiserikali ya Twaweza, ambao ulitaka kujua kama wananchi wana uchu wa mabadiliko na kama wanashiriki na wanaweza kuiwajibisha serikali.

Akizungumza katika uzinduzi wa ripoti hiyo iliyofanyika jijini Dar es Salaam jana, Mwakilishi wa Twaweza, Elvis Mushi alisema kutokana na hali hiyo wananchi waliweza kueleza moja kwa moja namna ambavyo taasisi hizo zinavyoshindwa kuwajibika kwao.

Alisema utafiti huo unaonyesha wananchi tisa kati ya kumi walisema hawajawahi kuzungumza au kuwasiliana na mbunge wao ndani ya kipindi cha mwaka mmoja na nusu uliopita.

Aidha asilimia 47 ya wananchi walisema hawajawahi kuzungumza na mwenyekiti wao wa mtaa, kijiji ili kujadili masuala yanayowahusu.

Kwa mujibu wa utafiti huo, wananchi saba kati ya kumi ambao ni sawa na asilimia 68, wanachangia moja kwa moja katika ujenzi au ukarabati wa vituo na majengo ya umma.

“Kati yao asilimia 88 walichangia fedha na waliobaki walichangia muda wao. Hata hivyo hatua hiyo haikulingana na viwango vya ukusanyaji wa kodi, lakini ilionyesha kuwa wananchi kwa njia moja au nyingine huchangia uendeshaji wa serikali,” alisema Mushi.

Alibainisha kuwa makusanyo mbalimbali ya wananchi hayaratibiwi vizuri kisheria kwa sababu michango haikusanywi kwa haki wala kutumika kwa tija kutokana na uwazi mdogo pamoja na mfumo dhaifu wa kudhibitiana.

Mkuu wa Twaweza, Rajani akitoa maoni juu ya matokeo hayo, alisema changamoto muhimu za utoaji huduma bado zipo kwenye sekta zote kuu na kama serikali haitakuwa sikivu zaidi, wananchi wanaweza kushuhudiwa wakiwa wakali zaidi katika siku zijazo.

Naye Mwenyekiti wa East Africa Speakers Bureau, Paul Mashauri, ambaye alikuwa mgeni rasmi, alisema serikali inapaswa kuzifanyia kazi tafiti zinazotolewa na wadau mbalimbali ili kuepusha athari ambazo zinaweza kujitokeza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles