30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali kuwashughulikia wanaoficha sukari

Charles MwijageVeronica Romwald na Florian Masinde, Dar es Salaam

SIKU chache baada ya gazeti la MTANZANIA Jumamosi kuripoti kile kilichoonekana wazi kuwa wafanyabiashara wa sukari nchini wameamua kuanzisha vita na Rais Dk. John Magufuli, kutokana na kuficha bidhaa hiyo na hivyo kuadimika katika soko na kupanda bei, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage ametangaza kuanza kuwachukulia hatua.

Mwijage ambaye alikuwa akizungumza na waandishi wa habari jana kuhusu kongamano la biashara kati ya Tanzania na Vietnam litakalofanyika kesho, alilazimika kuzungumzia suala hilo la sukari baada ya kuulizwa hatua ambazo watazichukua ili kukabiliana na kile kinachoonekana kuwapo kwa uhaba wa bidhaa hiyo.

“Nitafanya ukaguzi, na yule atakayebainika kuficha sukari nitakwenda kufunga ghala lake na katika hili simwogopi mtu yeyote,” alisema Mwijage.

Kauli hiyo ya Mwijage imekuja ikiwa zimepita siku 10 tu tangu Bodi ya Sukari nchini itoe tamko ikidai kubaini baadhi ya wafanyabiashara kuanza kufanya mipango ya kuhujumu utaratibu mpya uliotangazwa na Rais Magufuli.

Utaratibu huo mpya unataka uagizwaji wa bidhaa hiyo nje ya nchi ufanywe na wazalishaji, hatua ambayo inakata mrija wa ulaji wa wafanyabiashara hao.

Kama ambavyo Bodi ya Sukari ilidai, Mwijage naye aliwashutumu wafanyabiashara wa bidhaa hiyo kuficha sukari katika maghala yao ili ionekane kuna upungufu na hakuna uzalishaji wa kutosha nchini.

“Hakuna ‘crises’ ya sukari nchini kama ambavyo inadaiwa, mambo yapo vizuri, sukari ipo ya kutosha lakini kuna baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wakiificha ghalani ili ionekane kuna upungufu.

“Nitaanza kufanya ukaguzi wakati wowote kuanzia sasa na nitakwenda kwenye ghala fulani (bila kulitaja) ambalo tutalikagua na tukibaini ukweli tutalifunga mara moja,” alisema.

Mwijage alisema Serikali iliamua kupiga marufuku uingizwaji wa sukari kutoka nje ili kufanikisha lengo lake la kufufua na kuimarisha viwanda vya ndani.

“Na ndiyo maana tukapiga marufuku kuingizwa sukari ya nje ambayo nyingi ipo chini ya kiwango na inauzwa bei ya chini, sasa hatuwezi kujenga viwanda kwa mazingira hayo,” alisema.

Waziri huyo aliongeza kuwa tayari wawekezaji wengi wamejitokeza kushirikiana na Serikali kwa kujenga viwanda kwa ajili ya kuzalisha sukari.

“Kuna mwekezaji mmoja alitaka siku nyingi kuzalisha sukari, lakini hakukubaliwa, aliposikia uamuzi wa Serikali alikuja tumezungumza na hivi sasa atakwenda kujenga kiwanda mkoani Kigoma,” alisema.

Februari 18, mwaka huu, Rais Magufuli alipiga marufuku kiongozi yeyote wa Serikali kutoa kibali cha kuagiza sukari kutoka nje ya nchi na kwamba kitatolewa na yeye mwenyewe.

Akitangaza uamuzi huo, Magufuli aliwatuhumu baadhi ya wafanyabiashara waliopewa vibali hivyo kuvitumia kwa masilahi binafsi na hata kuwa chanzo cha kufa kwa viwanda vya sukari vya ndani.

“Mtu anaagiza sukari kutoka nje, tena wakati mwingine ni sukari ambayo muda wake wa kuisha matumizi umekaribia. Huyu mfanyabiashara anaingiza sukari hiyo na kuifungasha upya ili isijulikane kuwa inakaribia kuharibika na kuwauzia wananchi masikini.

“Kitendo hiki kinasababisha sukari inayozalishwa na viwanda vya ndani kukosa soko, wakulima wanakosa soko la miwa yao, na Serikali nayo inakosa mapato ya ushuru. Kwa vile bahati nzuri Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa) na Makamu wa Rais (Samia Suluhu Hassan) mpo hapa, nasema kuanzia sasa asiwepo mtu wa kutoa kibali cha mtu kuagiza sukari kutoka nje hadi ruhusa hiyo itoke kwangu,” alikaririwa Rais Magufuli wakati akitangaza utaratibu huo mpya.

Tangu Rais Magufuli atangaze msimamo huo, wananchi  wamekuwa wakilalamika kupanda kwa bei ya bidhaa hiyo, huku wafanyabiashara nao wakitoa sababu za kuadimika.

Mbali na hilo, Waziri Mwijage pia alisema Serikali kwa sasa inakimiliki kiwanda cha matairi cha General Tyre kwa asilimia 100 na kwamba kitaanza kufanya kazi hivi karibuni.

“Kilikuwa chini ya mwekezaji na alikuwa ana hisa asilimia 56, tumezichukua zote tunataka kifanye kazi ili wananchi walime zao la mpira na kiwanda kinunue na kuzalisha bidhaa,” alisema.

Kuhusu kongamano la Tanzania na Vietnam, Waziri Mwijage alisema litafanyika katika ukumbi wa mikutano wa Mwalimu Nyerere ambapo Rais wa Jamhuri ya Kisoshalisti ya Vietnam, Truong Tan Sang na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa watahutubia.

Alisema kongamano hilo ni fursa ya kuwakutanisha wafanyabiashara wa nchi hizo mbili ili kutengeneza mawasiliano ya kibiashara.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles